Kiongozi wa Wagner atishia kuondowa kikosi chake Bakhmut
5 Mei 2023Kiongozi wa kundi la kikosi cha mamluki kutoka Urusi,Wagner, Yevgeny Prigozhin ametangaza kwamba wapiganaji wa kikosi hicho wataondoka katika mji wa Bakhmut,walikokuwa wakiendeleza mapambano ya kuunyakuwa mji huo wa Ukraine tangu msimu wa joto ulipita.
Hivi sasa Prigozhin anasema wapiganaji wake wengi wameuliwa kwenye mapambano hayo na anataka kuondowa kikosi chake kutoka Bakhmut Mei 10.
Kiongozi huyo wa kikosi maalum cha wapiganaji wa kukodi amesema ukosefu wa silaha umesababisha maafa makubwa kwa wapiganaji wake katika uwanja wa vita kwenye mji huo wa Mashariki mwa Ukraine na kwahivyo hana budi bali kuondowa wanajeshi wake na kuwapeleka kwenye kambi maalum kujiuguza majeraha na kuziacha harakati hizo kwa vikosi vya serikali ya Urusi chini ya wizara ya ulinzi.
Tamko hilo limechapishwa leo Ijumaa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Telegram ingawa haikuwa bayana ikiwa taarifa hiyo ya Prigozhin inaweza kupewa uzito na hasa kutokana na kuonesha amekuwa huko nyuma, mara kwa mara akitowa matamko ya kukurupuka. Ni wiki iliyopita tu alilifuta tamko moja alilolitoa akidai kwamba alilitowa kama utani.
Tamko la hivi sasa limefuatiwa na kanda ya video iliyochapishwa hii leo akionekana mwenyewe Prigozhin akiwa amezungukwa na maiti chungunzima aliosema ni wapiganaji wa Wagner waliouwawa. Na kwenye mkanda huo alisikika akifoka kutowa ujumbe kwa waziri wa ulinzi Sergei Shoigu na mkuu wa majeshi jenerali Valery Gerasimov akisema ndio wanaopaswa kulaumiwa kwasababu waliwanyima silaha.
Katika upande mwingine wa mgogoro huo,inaonesha mapambano kati ya Ukraine na Urusi yalihamia Ankara hapo jana ambapo zilizuka ngumi kwenye ukumbi wa mkutano kati ya wajumbe wa nchi hizo.Mbunge wa Ukraine Oleksandr Marikovski alivaana na katibu wa Ujumbe wa Urusi Valery Stavitsky baada ya kuivuta na kuiondowa bendera ya Ukraine kwenye chumba cha mkutano. Vurugu hizo zilizuka katika mkutano wa wabunge wa nchi zinazopakana na bahari nyeusi uliofanyika katika mji mkuu wa Uturuki,Ankara.
Vidio hiyo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuchapishwa na mbunge wa Ukraine.Lakini pia hii leo Uturuki inatarajiwa kusimamia mkutano kati ya maafisa wa nchi hizo mbili Urusi na Ukraine mjini Istanbul kujadili suala la kurefusha muda wa makubaliano ya kuruhusu usafirishaji nafaka kutoka Ukraine kupitia bahari nyeusi.
Takriban miezi 15 baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulioiacha miji chungunzima ikiwa imeharibiwa na maelfu kuuwawa,bado hakuna mipango thabiti ya kusitishwa vita au kupatikana amani kwenye eneo hilo.
Ripoti za hivi punde zinasema moto umezuka kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta kusini mwa Urusi hii leo ikiwa ni siku moja baada ya maafisa wa nchi hiyo kuthibitisha kutokea shambulio la droni.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, amesema tukio linalodaiwa kuwa shambulizi la droni dhidi ya ikulu ya Kremlin lisingeweza kufanyika bila ya ufahamau wa serikali ya Washongton na kutowa onyo kwamba Urusi itajibu kwa kuchukua hatua kali.