Kiongozi wa upinzani Zanzibar Maalim Seif akamatwa
27 Oktoba 2020Kiongozi wa upinzani visiwani Zanzibar amekamatwa na watu watatu wameuwawa. Kwa mujibu wa maelezo ya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo leo Jumanne, kiongozi wake wa Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad amekamatwa wakati ambapo vurugu zimezuka katika visiwa hivyo kabla ya uchaguzi.
Maalim Seif Sharif Hamad anayewania nafasi ya urais wa Zanzibar amekamatwa na polisi baada ya kuwasili leo katika kituo cha kupigia kura katika eneo la Garagara ambapo alijaribu kupiga kura katika siku ya kwanza ya uchaguzi wa mapema ulioandaliwa kwa ajili hasa ya vikosi vya usalama.
Chama chake ACT Wazalendo kimeandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitta kwamba Hamad amekamatwa siku moja kabla ya uchaguzi wa rais na bunge utakaofanyika Zanzibar na bara hapo kesho Jumatano. Muda mfupi baada ya kukamatwa kwa Seif polisi walifyetua mabomu ya kutoa machozi na risasi na kumpiga kikatili mwanamume mmoja karibu na shule ya msingi ya Mtupepo ambako kuna kituo hicho cha kupiga kura na ambako ni ngome ya upinzani.
Mwandishi wa shirika la habari la AFP ameshuhudia matukio hayo. Upinzani unaamini kwamba kura hii ya mapema ya leo inayopigwa na vikosi vya usalama ni njama ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi visiwani Zanzibar. Zanzibar ina historia ya kushuhudia mivutano katika uchaguzi na upinzani umewatolea rai wafuasi wake kujitokeza kupiga kura leo.
Jana Jumatatu usiku vurugu zilizuka katika kisiwa cha Pemba ambako ni ngome kuu ya upinzani wakati jeshi likisambaza kura ambazo wafuasi wa upinzani wanaamini zimeshajazwa mapema.Chama hicho kinasema watu watatu wameuwawa na tisa wamejeruhiwa.