1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani wa Belarus akimbilia nchini Lithuania

Saleh Mwanamilongo
11 Agosti 2020

Svetlana Tikhanovskaya, anayepinga kuchaguliwa tena kwa rais Alexander Lukashenko,amekimbilia nchini Lithuania.Amesema waziri wa Mambo ya nje wa Lithuania.

https://p.dw.com/p/3gmd6
Waziri wa mambo ya nje wa Lithuania ,Linas Linkevicius amesema Bi Svetlana, amewasili Lithuania na yuko salama.
Picha: Reuters/V. Fedosenko

Mgombea wa urais kutoka kambi ya upinzani nchini Belarus Svetlana Tikhanovskaya, anayepinga kuchaguliwa tena kwa rais Alexander Lukashenko, amekimbilia nchini Lithuania. Taarifa hiyo imetangazwa leo na waziri wa Mambo ya nje wa Lithuania Linas Linkevicius. Tikhanouskaya mwenye umri wa miaka 37 aliibuka kuwa mpinzani mkuu wa Rais Lukashenko, akiwania uongozi baada ya mume wake kufungwa jela.

Linas Linkevicius amesema Bi Svetlana, amewasili Lithuania na yuko salama, huku maandamano dhidi ya ushindi wa rais wa Belarus, aliyechaguliwa kwa muhula wa sita, yakiwa yametawanywa na polisi kwa usiku wa pili mfululizo.

Hayo yanajiri wakati Umoja wa Ulaya umetilia mashaka matokeo ya uchaguzi nchini humo. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, ameitaka Belarus kutoa matokeo sahihi ya uchaguzi wa rais, baada ya rais Alexander Lukashenko kuibuka na ushindi mkubwa.

Kwa upande wake,Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaelezea wasiwasi wake kuhusu hali nchini Belarus. Msemaji wake Stéphane Dujarric amesema kwamba katibu mkuu wa umoja wa mataifa ametoa mwito serikali kujizuwia na matumizi ya nguvu.

''Katibu mkuu anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali inavyoendelea nchini humo, zikiwemo ripoti za maandamano ya baada ya uchaguzi na matumizi ya nguvu mjini Minsk na kwenye miji mingine. Katibu mkuu anawatolea mwito viongozi wa Belarus kujizuwia na matumizi ya nguvu na kuhakikisha uhuru wa kujieleza."

Ulaya na Marekani zaikosoa Belarus

Waandamanaji zaidi ya 3000 wakamatwa na polisi mnamo siku mbili ya maandamano.
Waandamanaji zaidi ya 3000 wakamatwa na polisi mnamo siku mbili ya maandamano.Picha: Reuters/V. Fedosenko

Rais Lukashenko alishinda uchaguzi wa rais kwa asilimia 80 ya kura na kupongezwa na jirani yake, Rais wa Urusi Vladmir Putin, lakini mataifa kadhaa ya Magharibi yameonyesha wasiwasi juu ya ushindi wake.

Awali rais Lukashenko aliwaambia raia wa taifa hilo kwamba hakutatokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Belarus kwa kuwa amejipanga kuzuia majaribio yote ya kuidhoofisha serikali yake.

Usiku wa Jumatatu mamia ya raia waliandamana mjini Minsk ambako walijaribu kuweka vizuwizi barabarani. Polisi imesema mtu mmoja amefariki. Kwa mujibu wa polisi ni kwamba mtu huyo alifariki wakati kilipuzi alichokuwa amekishikilia mkononi kulipuka.

Ikulu ya Marekani imesema ina wasiwasi mkubwa na kuongeza kwa ukandamizaji wa wagombea wa upinzani na kuwafunga waandamanaji walioandamana kwa amani.Ujerumani ilielezea uwezekano wa kuiwekea vikwazo Belarus,huku Urusi na China zikimpongeza rais Lukashenko kwa ushindi wake.