Tihkanovskaya awasilisha ombi la muingilio wa UN nchini humo
18 Septemba 2020Akihutubia kikao maalumu cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video, Tikhanovskaya amesema kuwa ukatili na nguvu ya kupitiliza inayotumiwa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya wafuasi wa upinzani ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kimataifa na azimio la pamoja la haki za binadamu lililoidhinishwa na Umoja wa Mataifa.
Tikhanovskaya pia ameliambia baraza hilo kuwa matakwa yao ni rahisi na yanaambatana na kanuni zote za kimsingi za kimataifa.Amesema wanataka kusitishwa mara moja kwa ghasia dhidi ya raia wapenda amani, kuachiwa huru mara moja kwa wafungwa wote wa kisiasa, uhuru wa mchunguzi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Belarus na hatimaye uchaguzi huru na haki ili raia wa Belarus waweze kuchagua kwa njia huru serikali yao kulingana na sheria za nchi hiyo.
Baraza hilo la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa liliandaa kikao hicho cha dharura licha ya wanadiplomasia kutoka Belarus na washirika wake wa karibu kujaribu kuzuia ripoti kuhusu ukiukaji kuwasilishwa katika mkutano huo wa Geneva. Naibu kamishna mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Nada al- nashif, ameliambia baraza hilo kwamba kumekuwa na maelfu ya visa vya kukamatwa , mamia ya ripoti za mateso yanayowajumuisha watoto pamoja na matukio ya utekaji nyara huku maandamano yakiendelea dhidi ya kuteuliwa kwa Lukashenko kuhudumu uongozini kwa awamu ya sita.
mipaka ya Belarus yasalia wazi
Wakati huo huo, mipaka ya Belarus leo Ijumaa imesalia wazi licha ya rais Lukashenko kutangaza kuwa itafungwa na kuonya kuhusu uwezekano wa ''vita'' na mataifa jirani anayoyatuhumu kwa kuunga mkono wimbi la upinzani nchini humo.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa telegram, huduma ya ulinzi wa mipaka imesema kuwa mikakati yote ya uangalizi imeimarishwa na maafisa wa usalama wa ziada kupelekwa katika vituo vya ukaguzi lakini watu wanaruhusiwa kuingia na kutoka nchini humo.
Siku ya Alhamisi, Lukashenko ambaye ameliongoza taifa hilo kwa muda wa miaka 26, alikiambia kikao cha wanawake kwamba maafisa wa jeshi watapelekwa katika mipaka kati ya nchi hiyo na Lithuania, Latvia, Poland na Ukraine. Hata hivyo waziri mkuu wa Lithuania Saulius Skvernelis amepuuza matamshi ya Lukashenko kuhusu vita na kuyaita ''kelele'' huku akisema ''hakuna uamuzi'' uliochukuliwa kufunga mipaka hiyo.