1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani ashinda Somaliland

Aboubakary Jumaa Liongo2 Julai 2010

Kiongozi wa upinzani katika eneo lililojitenga na Somalia , Somaliland,Ahmed Mohamed Silanyo ametangazwa kuwa mshindi kama ilivyotegemwa na wengi katika uchaguzi mkuu wa urais wa wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/O8oS
Hargeisa, SomalilandPicha: DW/Richard Lough

Somaliland ambayo ilaitawaliwa na Uingereza wakati ambapo sehemu iliyobakia ya Somalia ilitawaliwa na Italia, ilijitangzia uhuru wake mwaka 1991.Kwa upande mwengine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameitaka Somalia ambayo inaadhimisha miaka 50 ya uhuru wake, kutafuta njia za kurejesha umaoja.

Matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Somaliland yanaonesha kuwa kiongozi huyo wa chama cha upinzani Tulmiye Unity amepata 49.59 asilimia ya kura zilizopigwa, wakati ambapo Rais Dahir Rayale Kahin amepata 33.23 asilimia.Chama cha Haki na Jamii kilipata asilimia 17.18 na kukiri kushindwa.

Kiasi ya watu millioni 1 na elfu 9 walijiandikisha kupiga kura miongoni mwa raia millioni tatu unusu wa eneo hilo, ambapo waliyoweza kupiga kura walikuwa ni laki tano na elfu 38.Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Somaliland Essa Yusuf Mohammed amesema uchaguzi huo ni muhimu kwa wananchi wa eneo hilo na pia ni hatua moja kubwa kuelekea demokrasia kamili.

Rais huyo mteule wa Somaliland Ahmed Mohamed Silanyo, katika uchaguzi uliyopita mwaka 2003, alishindwa na Rais Kahin ambaye alipata asilimia 80 ya kura zote.Kwa mujibu wa katiba ya Somaliland, mahakama kuu inatakiwa kuthibitisha matokeo ndani ya kipindi cha siku 15 baada ya kutangazwa.

Waangalizi wa kimataifa walisema kuwa uchaguzi huo, ulikuwa huru na wa haki, pamoja na kwamba kulikuwa na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza, kama vile chama tawala kutumia fedha za serikali pamoja na magari na vyombo vya habari vya serikali katika kampeni.

Somaliland ambayo bado haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa nchi inayojitawala, zaidi ya kutambuliwa na Yemen tu, inajiweka mbali na Somalia ambayo imeshuhudia miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ban Ki-moon auf Kopenhagener Klimagipfel
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaBan Ki-moon ametumia nafasi ya kuadhimisha miaka 50 tokea kwa Somalia yote kujipatia uhuru wake, kutoa wito kwa nchi hiyo kutafuta njia za kurejesha umoja.

Ban Ki-moon amepongeza ushapavu na ujasiri wa wananchi wa Somalia na kuwathibitishia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwasaidia kukabiliana na kuzishinda changamoto kubwa walizonazo na kufikia ndoto ya kuwa na maisha ya amani, utulivu na mustakhbali mzuri.

Katika taarifa yake hiyo amewataka wasomali wageuke nyuma na kuangalia zama ambazo wananchi wa nchi hiyo miaka 50 iliyopita walishikamana kwa hari na fahari wakiwa na mategemeo ya kuwa na taifa lao ima

Serikali ya Rais Sheikh Sharif Ahmed inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na ambayo inadhibiti maeneo machache katika mji mkuu Mogadishu, inaadhimisha sherehe hizo za miaka 50 ya uhuru.Hata hivyo maadhimisho hayo yalishuhudia watu 17 wakiuawa katika mapigano kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa kiislam.

Mapema Kundi la wanamgambo wa kiislam la Heb Al-Islam limewataka raia kususia maadhimisho hayo na kuonya kuwashambulia wale watakaoshiriki.

Somalia Mogadischu Islamisten Flüchtlinge
Maiti ya raia aliyeuawa katika mapigano ikipelekwa katika hospitali ya Medina mjini MogadishuPicha: AP

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha matibabu ya dharura mjini Mogadishu, Ali Muse, watu 11 wakiwemo watoto watano na wanawake watatu waliuawa baada ya kombora kulipua jengo moja.

Kituo cha radio kinachomilikiwa na serikali kilitangaza kuwa Rais Sheikh Sharif Ahmed amekwenda mstari wa mbele kwenye mapambano na wanamgambo hao wa kiislam.Picha za televisheni zilimuonesha kiongozi huyo akiwa katika mavazi ya kijeshi kwenye eneo la mapambano.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/DPA

Mhariri:Josephat Charo