Kiongozi wa Taliban auawa nchini Pakistan
2 Novemba 2013Kifo hicho ni pigo kubwa kwa kundi hilo na kimetokea baada ya serikali kusema imeanzisha mazungumzo ya amani na wanamgambo. Mehsud alikuwa kwenye orodha ya wahalifu wanaosakwa na Marekani huku kukiwa na zawadi ya dola milioni tano kwa yeyote ambaye angetoa maelezo kuhusu mahali aliko. Anaaminika kuwa ndiye aliyepanga shambulizi la kujitoa mhanga katika kambi ya shirika la ujasusi la Marekani CIA nchini Afghanistan, tukio lililoshindikana la ulipuaji wa bomu la kutegwa ndani ya gari katika eneo la New York Time Square na mashambulizi mengine nchini Pakistan ambayo yamewauwa maelfu ya raia na wanajeshi.
Kamanda huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye alikuwa na ushirikiano wa karibu na al-Qaeda aliripotiwa kuwa aliuawa mnamo mwaka wa 2010, kabla ya kuibuka tena baadaye. Lakini afisa wa kijasusi wa ngazi ya juu nchini Marekani amesema jana kuwa Marekani imepokea uthibitisho kuwa Mehsud ameuawa.
Maafisa wawili wa kijasusi wa Pakistan pia wamethibitisha kifo chake, pamoja na makamanda wawili wa Taliban ambao waliuoana mwili wake ulioharibika vibaya baada ya shambulizi hilo. Kamanda wa tatu amesema Taliban huenda ikamchagua mrithi wa Mehsud hii leo Jumamosi.
Aliyekuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA ambaye alistaafu mwezi Agosti Michael Morell amesema kuwa kama ni kweli Hakimullah Mehsud ameuawa, litakuwa pigo kubwa sana kwa Taliban, kundi ambalo ni kitisho kikubwa kwa waPakistan na Wamarekani walioko Pakistan.
Pamekuwepo na ongezeko la mvutano baina ya Pakistan na Marekani kuhusiana na mashambulizi yanayofanywa na ndege zisizoruka na rubani, na Pakistan pia inajaribu kusaini mkataba wa amani na Taliban. Naibu kiongozi wa kundi hilo aliuawa katika shambulizi la ndege isiyoruka na rubani mwezi Mei, na mmoja wa manaibu wakuu wa Mehsud alikamatwa nchini Afghanistan mwezi uliopita wa Oktoba.
Maafisa wa ujasusi pamoja na makamanda wa kundi hilo la wanamgambo wamesema shambulizi lililomuua Mehsud lilifanywa katika makaazi ya kijiji cha Dande Derpaa Khel, katika eneo la kikabila la Waziristan ya Kaskazini. Wapiganaji wengine wanne waliuawa katika shambulio hilo ikiwa ni pamoja na binamu yake, mjomba na mmoja wa walinzi wake. Hawakutoa maelezo kumhusu mhanga wa nne. Karibu makombora manne yalirushwa baada tu ya gari ambalo Mehsud alikuwa ndani kuingia katika makaazi hayo, akitoka katika msikiti ulio karibu ambako maafisa wakuu wa Taliban walikuwa wakijadili kuhusu mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo