1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa muda wa Guinea asema Camara anahitaji muda zaidi kurejea hali yake ya kawaida.

Halima Nyanza7 Januari 2010

Kiongozi wa Muda wa guinea Sekouba Konate ameahidi kuandaa utaratibu utakaofungua njia ya kurudishwa kwa utawala wa kiraia na kutangaza pia kwamba kiongozi wa nchi hiyo, kapteni Camara anahitaji muda zaidi kupona.

https://p.dw.com/p/LN2Z
Kiongozi wa Kijeshi wa Guinea, kapteni Moussa Dadis Camara,ameelezwa kuwa anahitaji muda zaidi kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida.Picha: AP

Kauli hiyo ya Sekouba Konate ambaye kwa sasa anakaimu ukuu wa nchi, aliyoitoa wakati akizungumza katika televisheni ya taifa, inaashiria wazi kwamba mustakabali wa kisiasa wa Kapteni Camara, uko mashakani baada ya shambulio hilo la kutaka kumuua lililotokea Desemba 3.

Hata hivyo, Konate ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, amesema kapteni Camara hayuko katika hali mbaya, lakini anahitaji muda, utulivu zaidi pamoja na huduma ya afya itakayochukua muda ili aweze kupona kabisa.

Amesisitiza kuwa kwa sasa wanahitaji vitendo kuweza kurejesha amani na umoja wa kitaifa pamoja na kuiweka nchi hiyo na mfumo wake wa siasa katika msingi mpya.

Aidha kiongozi wa muda wa Guinea, Sekouba Konate ameahidi pia kumkubali Waziri Mkuu wa nchi hiyo atakayetoka upande wa upinzani ikiwa kama sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Amesema pia anatarajia serikali ya mpito kupanga tarehe mpya ya uchaguzi, baada ya iliyokuwa imepangwa awali kucheleweshwa kutokana na mzozo uliopo.

Kapteni Camara ambaye sasa yuko katika matibabu nchini Morocco, alishika madaraka kuiongoza Guinea kufuatia mapinduzi yaliyotokea Desemba mwaka 2008 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Lansana Conte, hayaonekana hadharani kwa zaidi ya mwezi sasa tangu alipopelekwa nchini humo, baada ya jaribio la kutaka kumuua la Desemba 3, ambalo lilifanywa na msaidizi wake wa zamani.

Kiongozi huyo aliwakatisha tamaa wa Guinea wengi pale alipokataa kujitoa katika uchaguzi, kuvunja ahadi alizozitoa muda mfupia baada ya mapinduzi yaliyomuweka madarakani.

Uongozi wa kapteni Camara uliingia matatani zaidi, kimataifa baada ya vifo vya raia zaidi ya 150, waliouawa na majeshi ya serikali, wakati wakiupinga utawala huo.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Morocco imeipokea kauli hiyo ya Kiongozi wa muda wa Guinea ya kumchagua haraka Waziri Mkuu kuongoza serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa na kufahamisha kwamba, Kapteni Camara yupo katika uangalizi maalumu kimatibabu.

Kiongozi wa muda wa Guinea, alimtembelea Kapteni Camara hospitali na akiwa mjini Rabat, alikutana kwa mazungumzo na wanadiplomasia wa Marekani na Ufaransa, ambao walimtaka aruhusu kurudishwa kwa utawala wa kiraia.

Wanadiploasia wa nchi za magharibi walioko katika mji mkuu wa Morocco, Rabat wanasema wanaamini kuwa Morocco imeiunga mkono Ufaransa na Marekani kumuondoa kapteni Camara, Guinea na kuimarisha juhudi na kuurejesha utawala wa kiraia katika kipindi hiki ambacho kiongozi huyo hayupo.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema mabadiliko yasiyo ya kikatiba ya serikali na matendo yasiyo ya kidemokrasia, yanatishia amani na uimara wa Afrika magharibi.

Ban Ki Moon ameyataja mapinduzi ya kijeshi na mauaji ya wapinzani nchini Guinea, mzozo kuhusiana na katiba huko Niger, kuongeze kwa hali ya wasiwasi na wapinzani kutishia kugoma katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Rais nchini Togo na kuchelewesha tena kupanga tarehe ya uchaguzi nchini Ivory Coast, kumekuwa kukitishia amani ya eneo hilo la Afrika magharibi.

Mwandishi: Halima Nyanza(ap, reuters, afp)

Mhariri: Aboubakary Liongo