Kiongozi wa jimbo la Catalonia akubali uchaguzi mpya
31 Oktoba 2017Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels Puigdemont amesema alikuwa hatafuti hifadhi ya kisiasa nchini Ubelgiji baada ya mwendesha mashitaka mkuu wa serikali ya Uhispania kutaka afunguliwe mashitaka ya uasi na uchochezi.
Alipoulizwa na waandishi wa habari ni muda gani anatarajia kusalia Ubeligiji Puigdemont amesema hali inabadilika kila mara nchini Uhispania na kuwa kwa sasa nchini Ubeligiji wamehakikishiwa juu ya haki zao za msingi na kuwa wanatekeleza mipango yao vizuri kutokea nchini humo na kusisitiza kuwa hakwenda Ubeligiji kutafuta hifadhi ya kisiasa bali ni kwa ajili ya usalama wake na kwa vile Brussels ni makao makuu ya Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa pamoja na kuwa atarejea nchini mwake baada ya kuhakikishiwa usalama na mazingira huru yeye binafsi pamoja na viongozi wenzake.
Puigdemont amesema pia kuwa atakubaliana kwa nguvu zote na changamoto zitakazotokana na uchaguzi wa mapema ulioitishwa Desemba 21 na kusema wananchi wa Catalonia watashiriki uchaguzi huo na kusisitiza kuwa hatua ya serikali ya Uhispania kujaribu kuzuia mchakato wao wa kisiasa haitafanikiwa.
Hatua ya Puigdemont kusema kwamba atakubaliana na uchaguzi huo wa mapema katika jimbo la Catalonia mnamo Desemba 21 inathibitisha kuwa serikali kuu ya mjini Madrid imepata mafanikio katika juhudi za kukwamisha mchakato wa jimbo hilo kutaka kujitenga.
Jitihada za jimbo la Catalonia kujaribu kuzuia serikali ya mjini Madrid kutawala moja kwa moja jimbo hilo zimeonekana kugonga mwamba tangu mwanzoni mwa wiki hii na kuifanya iliyokuwa serikali ya jimbo hilo kuwa katika wakati mgumu.
Mahakama ya katiba yazuia tangazo la uhuru wa jimbo la Catalonia
Mahakama ya katiba ya Uhispania hii leo imezuia tangazo la uhuru wa jimbo la Catalonia lililotolewa na bunge la jimbo hilo Ijumaa iliyopita hatua ambayo haikudumu na kufutiliwa mbali katika muda usio zidi nusu saa.
" Ninatoa mwito kwa watu wa jimbo la Catalonia kujiandaa kwa mchakato mrefu kufikia demokrasia ambao ndio utakao kuwa msingi wa ushindi wetu" amesema Puidemont.
Serikali ya Uhispania tayari imekwishatamka kuwa Puigdemont anakaribishwa kushiriki katika uchaguzi wa Desemba 21 ulioitishwa na waziri mkuu Mariano Rajoy kama njia moja wapo ya kutatua mkwamo uliopo.
Mgogoro huo wa kisiasa mbaya zaidi kutokea nchini humo katika kipindi cha miongo minne tangu nchi hiyo irejee katika utawala wa kidemokrasia mwishoni mwa miaka ya 1970 umesababishwa na kura ya maoni iliyofanyika katika jimbo hilo la Catalonia Oktoba 1.
Licha ya kura hiyo ya maoni iliyoitikiwa na watu wasio zidi nusu ya wanaostahili kupiga kura na kutangazwa na mahakama ya Uhispania kuwa ni batili bado iliyokuwa serikali ya jimbo hilo inasisitiza kuwa inalipa mamlaka ya kutangaza uhuru wa jimbo hilo.
Mataifa ya ulaya ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa yameungana na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy na kukataa hatua ya jimbo la Catalonia kujitangazia uhuru ingawa baadhi wametoa mwito wa kufanyika majadiliano kati ya pande hizo mbili.
Mwandishi: Isaac Gamba/rtre
Mhariri : Gakuba, Daniel