1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kramp-Karrenbauer kutogombea nafasi ya Kansela

Angela Mdungu
10 Februari 2020

Annegret Kramp-Karrenbauer, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha CDU cha kansela wa Ujerumani Angela Merkel hatogombea nafasi ya kansela katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao

https://p.dw.com/p/3XYxL
Deutschland CDU-Chefin fordert von SPD und Grünen neuen Kandidaten in
Erfurt
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Kappeler

Tangazo hilo la AKK aliyekuwa akitazamiwa kumrithi Merkel linatajwa kuzidi kuukuza mgogoro katika chama chake wakati kikipambana kupata muafaka juu ya hatma ya mwelekeo wake wa kisiasa  baada ya kupoteza kura kwa chama cha Mrengo wa kulia cha AfD.

Msemaji wa Kansela Merkel Steffen Seibert amesema kuwa Kansela Merkel anaendelea kushikilia msimamo wake kuwa hatogombea mhula wa tano ifikapo mwaka 2021.

Karrenbauer anatarajiwa kuratibu mchakato wa kumpata mgombea mpya wa nafasi hiyo ifikapo  majira ya joto mwaka huu na kisha ataondoka madarakani kama kiongozi wa chama. Kati ya majina ya wanaotajwa kumrithi Karrenbauer kama viongozi wa chama ni pamoja na waziri wa afya Jens Sphan na Friedrich Merz, ambao walishindwa na Karrenbauer katika kinyang'anyiro cha kugombea uenyekiti wa chama hicho Desemba 2018. Waziri kiongozi wa jimbo la North Rhine-Westphalia Armin Laschet naye anatajwa kuwa huenda akawania nafasi hiyo. 

Mashaka juu ya uwezo wa Karrenbauer

AKKamekuwa akitiliwa shaka juu ya uwezo wake wa kumrithi Merkel ambaye ameiongoza Ujerumani kwa miaka 15. Wiki iliyopita, uwezo wa Kramp -Karrenbauer kudumisha nidhamu katika chama chake cha CDU katika jimbo la Thuringia la mashariki mwa nchi hiyo uliingia dosari.

Angola Merkel bietet Angola Unterstützung an
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Tawi la CDU jimboni humo lilidharau hatua yake ya kumuunga mkono kiongozi wa eneo hilo aliyesaidiwa na chama mbadala cha Ujerumani AfD  kinachopinga wahamiaji kuingia madarakani.  Jambo hili lilivunja makubaliano ya kutokushirikiana na chama hicho cha mrengo wa kulia.

Uamuzi wa Kramp- Karrenbauer wa kutogombea nafasi ya kansela unaacha swali kubwa kuhusu hatma ya Ujerumani ambayo uchumi wake unashikilia nafasi ya nne kwa ukubwa duniani  una dalili za kudhoofika. Hayo yanaendelea pia wakati Umoja wa Ulaya ukipambana kuimarika baada ya Uingereza kujiondoa.