1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Bavaria akataa kumfuta kazi naibu wake

Sylvia Mwehozi
3 Septemba 2023

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria la Ujerumani Markus Söder amethibitisha kuwa hatomfuta kazi naibu wake Hubert Aiwanger juu ya kashfa ya chuki dhidi ya Wayahudi.

https://p.dw.com/p/4VteE
Hubert Aiwanger
Hubert Aiwanger mwanasiasa aliyeandamwa na kashfa ya chuki dhidi ya Wayahudi katika siasa za UjerumaniPicha: Uwe Lein/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria la Ujerumani Markus Söder amethibitisha kuwa hatomfuta kazi naibu wake Hubert Aiwanger juu ya kashfa ya chuki dhidi ya Wayahudi iliyopewa uzito katika siasa za Ujerumani kwa siku kadhaa.

Söder amekuwa chini ya shinikizo kubwa tangu wiki iliyopita kuamua ikiwa amfute kazi naibu wake huyo baada ya kuhusishwa kwenye  kipeperushi cha chuki dhidi ya Wayahudi wakati alipokuwa mwanafunzi siku za nyuma. Söder ameeleza kuwa amezungumza kwa kina na naibu wake kabla ya kufikia maamuzi hayo akiongeza kuwa kumfuta kazi si hatua sahihi.

Siku ya Alhamisi Aiwanger aliomba msamaha katika taarifa fupi, akisema anajuta sana kuwaumiza wengine kwa matendo yake wakati alipokuwa kijana lakini alikataa kujiuzulu.

Mwanasiasa huyo ni kiongozi wa chama cha Free Voters, na si kutoka Chama cha kihafidhina cha CSU, kinachoongoza siasa za Bavaria.