1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa al Shabaab atajwa kuuwawa

Admin.WagnerD4 Februari 2015

Maafisa wa Marekani wanasema kiongozi mwandamizi wa kundi lenye itikadi kali la Kiislamu la al-Shabaab nchini Somalia anaweza kuwa ameuwawa katika shambulizi la angani la jeshi la Marekani.

https://p.dw.com/p/1EVKS
Somalia Mogadischu Autobombe 4.1.2015
Shambulio la gari katika siku za hivi karibuni mjini MogadishuPicha: picture-alliance/dpa/Said Yusuf Warsame

Katika eneo la kusini la taifa hilo, kufuatia operesheni iliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, John Kirby, alisema kundi la mkuu wa operesheni za nje wa kundi la al-Shabaab lilishambuliwa na kombora la angani, lililotekelezwa na kikosi maalumu cha Marekani kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani na makombora mengine.

Hata hivyo bado hakujawa na taarifa rasmi za kuuwawa kwa kiongozi huyo anayetajwa kwa jina la Yusuf Dheeq. Na kwamba serikali ya Marekani imekuwa ikifuatilia kwa karibu ili kujua ukweli wa utekelezaji wa tukio hilo la matokeo yake kwa hivi sasa.

Maafisa wengine wanasema Dheeq ameuwawa katika shambulio hilo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Kirby anasema Dheeq amekuwa akihusika moja kwa moja katika kupanga na kufanya mashambulizi nje ya Somalia. Na kuongeza kama itathibitika kuwa ameuwawa, hilo litakuwa pigo lingine kubwa kwa kundi la al Shabaab.

Somalia Abdi Godane al-Shabaab Führer
Marehemu Abdi Ahmed Godane aliyekuwa kiongozi wa al ShabaabPicha: Rewards for Justice/AFPGetty Images

Aidha Kirby aliongeza kusema Marekani inaendelea kuwawinda viongozi wa al-Shabaab kwa sababu, kundi hilo ni mtandao wa kigaidi wenye mafungamano na al-Qaeda, ambalo linatishia usalama katika maeneo ya Afrika na kwa masilahi ya Marekani. Hakuna athari zozote zilizoanishwa kwa raia wa kawaida katika operesheni hiyo.

Maafisa wa Serikali ya Somalia na wengine walioshuhudia waliliambia shirika la habari la AFP siku hiyo ya Jumamosi waliiona nyumba ambayo inatumiwa na wanachama wa kundi hilo la al-Shabaab ikishambiliwa na kombora la angani.

Maafisa wa Marekani wamesema mtu mmoja aliuwawa katika shambulizi hilo. Wanasema shambulizi lilifanyika karibu na mji wa Dinsoor katika eneo la ufukwe kusini magharibi. Maafisa walitoa taarifa hiyo kwa masharti ya kutotajwa majina yao kutokana na kutoruhusiwa kusema lolote kwa umma kwa utataratibu wa majukumu yao.

Taarifa rasmi kutoka Marekani zinasema kuna takribani washauri wa kijeshi 100 nchini Somalia, lengo likiwa kuisaidia serikali ya taifa hilo kukabiliana na al-Shabaab. Kundi hilo limekuwa likipigana kuiondoa madarakani serikali ya Somalia inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa lakini vile vile limekuwa likifanya mapambano ya kulipiza kisasi katika mataifa jirani.

Marekani imekuwa ikiwalenga viongozi wa al-Shabaab, katika mfululizo wa mashambulizi yake katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka uliopita, wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilithibitisha kwamba mashambulizi ya angani ya jeshi la taifa hilo yalimuua mkuu wa upelelezi wa al-Shabaab, Tahlil Abdishakur.

Na katika mkasa mwingine unaofanana na huo Septemba mosi mwaka huo huo Marekani ilitihibitisha kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo Ahmed Abdi Godane.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/APE

Mhariri:Josephat Charo