Kiongozi mwengine wa al-Qaeda Al - Libi auawa?
6 Juni 2012Maafisa wa Marekani wamethibitisha kwamba Abu Yahya al-Libi aliuawa kutokana na shambulio la kombora lililofyatuliwa kutoka kwenye ndege ya Marekani inayoruka bila ya rubani. Shambulio hilo lilifanyika ndani ya Pakistan.
Al-Libi aliekuwa mpambe mwaminifu wa kiongozi wa hapo awali wa mtandao wa al-Qaeda, Osama bin Laden, ni raia wa Libya aliekuwa anatokea mara kwa mara katika kanda za video . Alihesabika kuwa injini ya propaganda ya mtandao wa al-Qaeda. Ikulu ya Marekani imesema kifo cha al-Libi ni pigo kubwa kwa mtandao wa al-Qaeda, baada ya kuuawa kwa aliekuwa kiongozi wa mtandao huo, Osama Bin Laden . Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney ameeleza kuwa kifo cha al- Libi ni pigo kubwa katika moyo wa mtandao wa al-Qaeda.
Marekani imesema kuwa al-Libi alikuwa muhimu kutokana na kuwa makamu wa Ayman al Zawahiri lakini idara za ujasusi zinasema kuwa mtu huyo aliyekuwa raia wa Libya alikuwa injini ya propaganda na kwamba pia alikuwa na sifa za ujuzi wa dini ambazo viongozi wengine wa al-Qaeda hawakuwa nazo.
Kazi alizokuwa anazifanya katika mtandao wa al-Qaeda zilibainika baada ya nyaraka kugundiliwa na makomando wa Marekani katika maficho ya Osama bin Laden ya Abbottabad wakati wa shambulio lililomuua kiongozi huyo nchini Pakistan mnamo mwezi Mei mwaka uliopita.
Al-Libi aliezaliwa Januari mosi manmo mwaka 1963 alikuwa anajulikana kidogo tu kama mhubiri,kabla ya ujasiri wake wa kutoroka kutoka kwenye jela ya Marekani Bagram nchini Afghanistan ufahamika mnamo mwaka wa 2005. Ujasiri wake wa kutoroka, haraka ulimjengea umuhumi katika mtandao wa al-Qaeda kwani mara kwa mara alitokea katika kanda za video
Wakati huo huo kuna taarifa nyingine zinazodai kwamba al-Libi siye alieuawa katika shambulio la asubuhi. Shirika la televisheni la al-jazeera limesema alieuawa alikuwa dereva wake.
Mwandishi:Mtullya abdu
Mhariri: Abdul-Rahman