Kiongozi wa Chad atangaza hali ya hatari kufuatia mafuriko
20 Oktoba 2022Mafuriko yameathiri pakubwa majimbo 18 kati ya 23 ya Chad. Rais wa mpito wa nchi hiyo Mahamat Idriss Deby amesema zaidi ya watu milioni ni wahanga wa mafuriko. Ameongeza kuwa hakuna mtu aliekufa kutokana na mafuriko hayo. Akilihutubia taifa, Deby amesema janga hilo limesababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
''Ninatangaza kwamba hali ya hatari itaanzishwa ili kudhibiti vyema maafa haya ya asili. Maafa haya, yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, ni moja ya maafa makubwa zaidi ambayo kanda hii imewahi kushuhudia kwa miaka mingi. Ikifanya kama kuzidisha maafa kwa jamii ambazo tayari zinajitahidi kuweka vichwa vyao juu ya maji. Chad, nchi yetu, haijasalimika katika hili. Hali inayoathiri sehemu kubwa ya nchi.", alisema Mahamat Idriss Deby.
Huduma za dharura
Kiongozi huyo amesema mafuriko tayari yameathiri zaidi ya hekari laki nne na hamsini elfu (450.000) za mashamba na mifugo 19,000. Maeneo yaliyo hatarini zaidi ni mji mkuu N'Djamena na viunga vyake, alisema rais Mahamat Deby akieleza kuwa hali hiyo inazidi kutia wasiwasi. Kwenye hotuba yake kwa taifa, amesema serikali yake inapaswa kutoa makaazi, mahitaji ya kimsingi na ulinzi wa afya kwa wahanga.
Chad ni nchi ya tatu maskini zaidi duniani, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unasema Wachad milioni 5.5 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu, wakati Benki ya Dunia inasema asilimia 42 ya wakazi milioni 16 wanaishi katika umaskini.
Ombi la msaada wa kimataifa
Rais huyo wa mpito amezitaka nchi rafiki na washirika wa kiufundi na kifedha kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na athari za mafuriko hayo. Chad ina mito miwili mikuu, Chari na Logone, ambayo inapita kupitia majimbo yake ya kusini na kumwaga maji katika Ziwa Chad, huko eneo la mpaka na Niger, Nigeria na Cameroon.
Mafuriko si ya kawaida wakati wa msimu wa mvua wa Chad, ambao kawaida huanzia mwezi Mei hadi Oktoba katika mikoa yake ya kusini. Lakini mwaka huu mvua ilikuja mapema na ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa.