Kinyang'anyiro cha urais wa FIFA chapamba moto
12 Februari 2016Kilabu maarufu za soka barani ulaya zinamuunga mkono Katibu mkuu wa Umoja wa vyama vya kandanda vya ulaya –UEFA Gianni Infantino, mswisi mwenye asili ya Kitaliani. Mwenyekiti wa kilabu bingwa ya Ujerumani Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge alisema kwamba kutokana na myo wa kandanda wanamuunga mkono Infantino.
Rummenigge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa vilabu vya Ulaya alikuwa akizungumza na Shirika la habari la Ujerumani dpa mjini Paris kandoni mwa mkutano mkuu wa umoja huo, akiongeza kwamba vilabu vya soka barani ulaya vina imani na infantino.
Infantino ni mmoja kati ya wagombea watano wanaowania kuchukua nafasi ya kuliongoza Shirikisho la kandanda la kimataifa kutoka kwake Joseph Blatter aliyefungiwa na kamati ya maadili, kutokana na kashfa ya hongo. Wagombea wengine ni Rais wa Shirikisho la soka la Asia Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa wa Bahrain, Makamu wa zamani wa Rais wa FIFA Mwana mfalme Ali Bin Al Hussein wa Jordan, Afisa wa zamani wa Shirikisho hilo la FIFA Jerome Champagne wa Ufaransa na mfanyabiasahra tajiri wa Afrika Kusini Tokyo Sexwale.
Mapema wiki hii Shirikisho la kandanda la Austraia na yale ya Jamhuri ya Czech, Poland, Hungary na Liechtenstein yamesema yatamuunga mkono infantino. Lakini haijafahamika wazi ikiwa wanachama wote 53 wa UEFA watamuunga mkono Infantino ambaye atahitaji wingi wa kura 105 kutoka mashirika 209 wanachama wa FIFA. Rais wa Shirikisho la kandanda la Liberia Mussa Bility ameripotiwa akisema mataifa yapatayo 26 yatapiga kura bila kuzingatia ushawishi kutoka kwa mgombea yeyote, lakini Liberia itamuunga mkono Mwana mfalme Ali , wakati Sudan Kusini imeahidi kumuunga mkono infantino.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohammed Khelef