KINSHASA: Waandishi wa habari wapokonywa vifaa vyao vya kazi
16 Septemba 2007Waandishi wa habari wanaovifanyia kazi vyombo vya habari vya mataifa ya kigeni na Afrika wamepokonywa vyombo vyao vya kazi na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mashariki mwa nchi hiyo.
Mwandishi mmoja wa habari kutoka Marekani anayelifanyia kazi gazeti la Christian Science Monitor, waandishi wawili wa habari raia wa Kongo wanaofanya kazi na shirika la habari la Marekani, VOA, na kituo cha radio cha Canal Afrique na raia wa Rwanda anayechangia habari katika gazeti la Kigali New Times, walikamatwa juzi Ijumaa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Sake, takriban kilomita 30 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma.
Waandishi hao wanne wa habari walikuwa wameripoti kuhusu mapigano katika eneo la Masisi kati ya majeshi ya serikali na waasi wanaoongozwa na jenerali muasi Laurent Nkunda.
Waandishi hao waliachiliwa baada ya kuhojiwa lakini vifaa vyao vinazuiliwa na wanajeshi wa Kongo. Jeshi la Kongo mkaoni Kivu Kaskazini halijasema lolote kuhusiana na kisa hicho.