1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinshasa. Makundi ya utetezi wa haki za binadamu yaonya kuhusu kuendewa kinyume haki za raia.

22 Julai 2006
https://p.dw.com/p/CG58

Makundi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameonya wiki hii kuwa haki za binadamu katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo DRC , zisifumbiwe macho wakati wa kampeni za uchaguzi wa kihistoria mwezi huu na kutoa wito wa kuchukua hatua za haraka kutoka serikali pamoja na vyama vya siasa.

Shirika la Human Rights Watch , katika ripoti iliyotolewa siku ya Ijumaa , limesema kuwa serikali ya Congo inapaswa kuchukua hatua za haraka ili kumaliza mzozo katika jimbo la kusini la Katanga ambako mamia ya watu wameuwawa na wengine zaidi ya 150,000 wamekimbia makaazi yao kutokana na mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa Mai Mai.

Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani limesema kuwa kushindwa kwa serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wanajeshi na wengine wanaohusika katika mauaji, ubakaji na mateso kwa raia katika jimbo la Katanga kunaweza kuendeleza ghasia zaidi na hali ya kutokuwa na usalama katika jimbo hilo la kusini.