KINSHASA : Karantini kwenye eneo la mripuko wa Ebola
11 Septemba 2007Shirika la Afya Duniani WHO leo limetowa tahadhari kwa kuomba kupatiwa madaktari zaidi na wataalamu wengine kwenda kusini mashariki mwa Congo kupambana na mripuko wa gonjwa la Ebola ambalo tayari limeuwa zaidi ya watu 160.
Wataalamu kutoka Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka tayari wamekuwa wakiwatibu wagonjwa lakini msaada zaidi unahitajika.Serikali ya Congo leo imeliweka eneo hilo katika karantini.
Ebola ambayo ni homa yenye kuambukiza kwa haraka na huuwa asilimia 90 ya waathirika wake hauna tiba na husababisha wagonjwa kuvuja damu ndani ya ngozi,fadhaa na viungo kushindwa kufanya kazi.
Kirusi cha gonjwa hilo kimeuwa takriban watu 450 katika Jamhuri ya Demokrasi ya Congo tokea mwaka 1976.