1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimetto avunja rekodi mbio za Marathon Berlin

29 Septemba 2014

Dennis Kimetto aweka rekodi mpya ya mbio za marathon mjini Berlin jana Jumapili(28.09.2014) , Wachezaji wa golf wa bara la Ulaya wanyakua tena ubingwa wa kombe la Ryder kati ya bara la Ulaya na Marekani.

https://p.dw.com/p/1DNG7
41. Berlin Marathon 28. Sept. 2014 Kimetto Weltrekord
Dennis Kimetto kutoka KenyaPicha: TOBIAS SCHWARZ/AFP/Getty Images

Mkimbiaji kutoka Kenya Dennis Kimetto ameshinda mpambano wa 41 wa mbio za marathon mjini Berlin kwa kutumia saa 2 dakika 2 na sekunde 57, akiwa mkimbiaji wa kwanza kumaliza mbio hizo chini ya saa mbili , na dakika 3.

Rekodi ya awali ya saa 2, dakika 3 na sekunde 23 iliwekwa na Mkenya pia , Wilson Kipsang mjini Berlin mwaka jana.

"Najisia vizuri kwasababu nimeweka rekodi mpya ya dunia. Nafurahi sana."

41. Berlin Marathon 28. Sept. 2014 Kimetto 26. Sept.
Dennis Kimetto amevunja rekodi ya marathon ya BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Amesema hivyo Kimetto mshindi wa mbio hizo za Marathon mjini Berlin alipoulizwa na waandishi habari kuhusu hisia zake katika ushindi wa mbio hizo. Na akaongeza "mashabiki walinifanya nijiamini na nilifikiri kwamba naweza kushinda."

Mshindi wa pili Emmanuel Mutai pia amevunja rekodi ya zamani akimaliza kwa saa 2 dakika 3 na sekunde 13 na anaamini inawezekana kukimbia marathon kwa chini ya saa mbili.

"Kutokana na kile nilichokiona leo, muda unapungua zaidi na zaidi. Kwa hiyo kama sio leo, inawezekana kesho," Mutai mwenye umri wa miaka 29 amesema. Huenda mara nyingine tunaweza kupata saa 2, dakika moja."

41. Berlin Marathon 28. Sept. 2014 Matebo Kebede
Wakimbiaji mjini BerlinPicha: Reuters/Thomas Peter

"Mbio zilikuwa ngumu tangu mwanzo. Lakini mwanzoni kasi ilikuwa chini ,mno. Kwa hiyo baada ya kufikia nusu ya mbio hizo tulijaribu kuongeza kasi na kwamba mwishoni tuliweza kupata matokeo mazuri. Mara nyingine natumai naweza kuwa mshindi wa kwanza".

Mutai amekimbia marathon hii kwa kasi zaidi katika historia kwa kutumia saa 2, dakika 3 na sekunde 2 mjini Boston mwaka 2011, licha ya kuwa haikuhesabiwa kuwa ni rekodi ya dunia kwasababu njia ya mbio hizo ilifikiriwa kuwa imenyooka sana na yenye mteremko.

Katika mbio za jana mjini Berlin Mutai aliweka rekodi ya dunia kwa kukimbia kilometa 30 kwa saa 1, dakika 27 na sekunde 37, akiipiku rekodi ya Patrick Makau ya hapo awali ya saa 1, dakika 27 na sekunde 38 ya mwaka 2011.

Abera Kuma wa Ethiopia alikuwa wa tatu katika mbio hizo akiwa mbele ya Wakenya Geofrey Kamworor na Eliud Kiptanui.

Tirfi Tsegaye kutoka Ethiopia ameshinda mbio hizo kwa upande wa wanawake kwa kutumia saa 2, dakika 20 na sekunde 18 , huku mkimbiaji mwingine kutoka Ethiopia Feyse Tadese akishika nafasi ya pili.

Timu ya bara la Ulaya ya mchezo wa golf imepata ushindi kwa mara nyingine tena katika kombe maarufu duniani la Ryder.

Ushindi wa timu ya bara la Ulaya dhidi ya Marekani mjini Gleneagles ulikuwa wa kuumiza sana , hususan baada ya matamshi ya Phil Mickelson mchezaji wa timu ya Marekani mwenye uzoefu mkubwa zaidi dhidi ya mchezaji mwenzake Tom Watson.

40th Ryder Cup in Schottland 2014 - Phil Mickelson
Phil Mickelson wa timu ya UlayaPicha: picture-alliance/dpa/Andy Rain

Ikilinganishwa na wachezaji wa timu ya Ulaya ambayo ina wachezaji kutoka Uingereza, Wales , Scotland , Ireland ya kaskazini, Uhispania, Ufaransa, Ujerumani , Sweden, Denmark na Ufaransa walikuwa na lengo moja tu la ushindi na kuwa pamoja wakiunganishwa na nahodha wao , Paul McGinley.

Na sasa katika soka na tunanze na Bundesliga.

Ilikuwa ni pambano la watani wa jadi la 145, kati ya Schalke na Borussia Dortmund nchini Ujerumani siku ya Jumamosi, ambapo pambano hilo huwa gumzo kubwa nchini Ujerumani , ambapo jeshi la polisi hutoa ulinzi maalum na wanasiasa hukaa chonjo kuona nini kitatokea. Mara hii mchezo huo ulimazika salama bila matukio ya kutia wasi wasi, lakini haukuisha salama kwa makamu bingwa wa ligi hiyo Borussia Dortmund , ambapo jioni hiyo walitoka vichwa chini baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao hao wakubwa Schalke 04.

Borussia Dortmund ambayo imeanza msimu huu kwa kusua sua, imeonesha udhaifu mkubwa katika ulinzi ambapo hadi sasa imefungwa mabao 11 na kufunga tisa, wakiwa na pointi saba kibindoni na katika nafasi ya 12. Schalke iliyoanza msimu huu pia kwa kusua sua kwa ushindi huo imechupa hadi nafasi ya kumi ikiipita Dortmund.

Hambuger SV Johan Djourou Lewis Holtby Tolgay Arslan Fußball
Hamburg SV bado inasumbuka kupata ushindiPicha: picture alliance/dpa/Peter Steffen

Mario Goetze alikuwa nyota kwa upande wa Bayern wakati mabingwa hao watetezi wakiendelea kuwa juu ya msimamo wa ligi kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya FC Kolon licha ya kuwa kikosi cha kocha Pep Guardiola hakikung'ara kama ilivyostahili. Bayern imefikisha sasa pointi 14 kutokana na michezo sita.

Borussia Moenchengladbach ambayo iko katika nafasi ya pili iliishinda Paderborn ambayo imepanda daraja msimu huu kwa mabao 2-1, wakati Bayer leverkusen ililazimishwa sare ya bila kufungana na Freiburg.

Hamburg SV ambayo ni timu pekee ambayo haijawahi kushuka daraja nchini Ujerumani ilikuwa hadi jana Jumapili ni timu pekee ambayo haijapata bao msimu huu. Licha ya kupata bao jana dhidi ya Eintracht Frankfurt lakini kigogo hicho cha soka la Ujerumani kilishindwa kutamba na kukubali kipigo cha mabao 2-1.

Mchezaji wa kati wa Hamburg SV Tolgay Arslan alikuwa na haya ya kusema.

"Tulicheza vizuri katika mchezo wote. Walikuja mara tatu katika goli letu, na wakapata bao safi kabisa. Tunaweza tu kushutumu, kwamba hatupati hata bao moja. Naamini kwamba tuliutawala mchezo huo kwa dakika 88 na hii ndio hali yetu. Tunaweza kufanya kile tunachotaka. Lakini ni lazima hali hii iendelee."

Diego Costa alipachika goli lake la nane katika ligi ya Uingereza , Premier League wakati viongozi wa ligi hiyo Chelsea ikiendelea na hali yake ya kutoshindwa kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Aston Villa.

Edin Dzeko aliufumania mlango mara mbili wakati mabingwa Manchester City ikipata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Hull City na kuchupa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi , point mbili nyuma ya Southmpton , iliyoishinda Queens Park Rangers kwa mabao 2-1.

Manchester United imesogea katika nafasi ya saba ikiwa imepata ushindi wake wa pili msimu huu chini ya kocha Luis van Gaal kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham United.

Arsenal na Tottenham Hotspurs , Liverpool na Everton ziliridhika na sare wakati mapambano ya watani wa jadi mjini London yakiishia kwa sare ya bao 1-1.

Nchini Uhispania , Barcelona na Real Madrid zimeendelea kufukuzana wakati timu zote hizo zikipata ushindi mwishoni mwa juma, ambapo Atletico Madrid haikuachwa nyuma ambapo iliiadhibu Seville kwa kuitwanga mabao 4-0.

Fußball Chelsea Diego Costa
Diego Costa mshambuliaji wa ChelseaPicha: Reuter/Toby Melville

Paris St.German ya Ufaransa inakabana kooo na Barcelona ya Uhispania kesho Jumanne katika mpambano ambao unatarajiwa kuwa wa vuta nikuvute wa Champions League katika uwanja wa Parc des Princes. Barca iliitoa Paris St German miaka miwili iliyopita kwa sheria ya goli la ugenini katika robo fainali na hali inaelekea kujirudia yenyewe, ambapo makocha Laurent Blanc na Luis Enrique walikuwa wachezaji wa Barca kuanzia mwaka 1996-97, na mshambuliaji wa PSG Zlatan Ibrahimovic bado ana donge na klabu hiyo baada ya kufurushwa mwaka 2010 baada ya msimu mmoja tu.

Ibrahimovic anauguza maumivu ya kifundo cha mguu lakini anataka sana kuwa fit wakati wa pambano hilo la kundi F.

Bayern Munich itakuwa mjini Moscow ikipimana nguvu na CSKA Moscow katika uwanja wa Khimki lakini uwanja huo kesho hautakuwa na watazamaji kutokana na shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA kuamua kuiadhibu CSKA kucheza mchezo mmoja bila mashabiki wake kutokana na tabia ya kibaguzi ya mashabiki wake wakati ikipambana na mashabiki wanaoonesha tabia ya kibaguzi barani Ulaya.

Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge amekasirishwa kwamba adhabu hiyo dhidi ya CSKA ina maana kwamba mashabiki wa timu hiyo pia hawawezi kwenda mjini Moscow kuipa nguvu timu yao.

Katika michezo mingine kesho mabingwa Real Madrid wanapambana na Ludogorets ya Bulgaria katika mchezo wa kundi B. Basel inakwaana na Liverpool ya Uingereza, wakati Atletico Madrid inataka kurejea katika dimba hilo baada ya kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Olympiacos Piraus kwa kuikaribisha Juventus Turin ya Italia , ambayo ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malmo katika kundi A.

Siku ya Jumatano viongozi wa ligi ya Uingereza Chelsea iko nyumbani kwa Sporting Lisbon baada ya kupata sare katika mchezo wa kundi G dhidi ya Schalke 04. Arsenal inaikaribisha Galatasaray ya Uturuki katika kundi D ambapo Borussia Dortmund ina lenga kumuondoa mdudu mbaya anayewafuata katika ligi ya Ujerumani Bundesliga kwa kupata ushindi dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji kufuatia ushindi mnono katika mchezo wa kwanza dhidi ya Arsenal.

Ngumi

Mpiganaji ngumi nyota kutoka Ufilipino Manny Pacquiao leo amepuuzia majigambo ya Floyd mayweather , akisema anamuonea huruma hasimu wake huyo Mmarekani na anamtaka kusoma biblia.

Pacquiao amewahakikishia mashabiki wake pia kwamba atacheza kwa dakika chache mchezo wa mpira wa kikapu wakati msimu mpya utakapoanza mwezi ujao hata kama anajifua kwa ajili ya mchezo mjini Macau mwezi Novemba dhidi ya Mmarekani ambaye hajawahi kushindwa Chris Algieri.

Bildergalerie Sport Highlights 2012
Floyd Mayweather(kulia)Picha: AFP/Getty Images

Katika vituko vya hivi karibuni, Mayweather , ambaye hajawahi kushindwa katika mapambano yake 47, ameweka picha kadhaa katika mtandao wa kijamii , akimuonesha Pacquiao akiwa ameangushwa chini katika mapambano yaliyopita. Ameongeza kuwa Pac Man amechacha hana kitu mfukoni anasubiri malipo.

Naam kwa taarifa hiyo mpenzi msikilizaji ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea ukurasa huu wa michezo jioni ya leo jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre , ZR

Mhariri: Iddi Ssessanga