1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Bopha chaua zaidi ya 200 Ufilipino

5 Desemba 2012

Idadi ya vifo vilivyotokana na Kimbunga Bopha kilichoikumba Ufilipino inazidi kuongezeka na imefikia watu 230, huku mamia ya watu wengine wakipotelea katika maporomoko ya ardhi na mafuriko.

https://p.dw.com/p/16vy4
Wakaazi wa mji wa Tagun wakiangalia mti uliong'olewa kabisa na Kimbunga Bopha.
Wakaazi wa mji wa Tagun wakiangalia mti uliong'olewa kabisa na Kimbunga Bopha.Picha: Reuters

Kimbunga Bopha chenye upepo wa kati wa kilomita 120 kwa saa kimepiga maeneo ya fukwe kaskazini mwa Palawan hii leo na katika miji mingine.

Maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na kimbunga hicho ni pamoja na maeneo ya pwani, mashamba na maeneo ya migodini katika jimbo la Mindanao, ambapo kimbunga Bopha kimeharibu makazi, na kusababisha maporomoko yaliyoleta mafuriko na kuua watu wapatao 230.

Gavana wa jimbo lililoathirika vibaya la Compostela huko Mindanao, Arthur Uy, amesema maji na matope kutoka milimani yaliingia katika majengo ya shule na kufunika mahakama, majengo kadhaa ya mjini na vituo vya afya ambako wananchi walikuwa wamepatiwa malazi ya muda . Idadi ya vifo katika jimbo hilo imefikia 150.

Gavana Uy ameliambia shirika la habari la Reuters katika mahojiano kwa njia ya simu kuwa '' Maji yalikuja ghafla na pasipo kutarajiwa , upepo ulikuwa mkali na kusababisha maisha ya watu kupotea'' alisema gavana huyo.

Kilimo na miundombinu yaharibiwa

Uharibifu wa kilimo na miundombinu katika jimbo la Compostela unakadiriwa kufikia Pesos bilioni 4 sawa na dola milioni 98, ikiwa ni baada ya kimbunga hicho kuharibu asilimia 70 hadi 80 ya mashamba hususan ya ndizi ambayo ni kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

Mama akimbeba mwanawe kukimbia madhara ya Kimbunga Bopha.
Mama akimbeba mwanawe kukimbia madhara ya Kimbunga Bopha.Picha: AFP/Getty Images

Karibu watu 60 wamepoteza maisha katika mji mpya wa Bataan pekee na wengine 245 bado hawajulikani walipo, amesema Gavana Uy akiongeza kuwa mawasaliano yamekatika kwa muda.

Ufilipino imekuwa ikikumbwa na vimbunga karibu 20 kwa mwaka na mara nyingi vimekuwa vikisababisha vifo na uharibifu mkubwa. Mwezi Disemba mwaka jana watu 1500 waliuawa na Kimbunga Wash katika jimbo la Mindanao.

Juhudi za uokoaji zinaendelea lakini vikosi vya uokoaji vinapamban ana hali mbaya ya hewa huku maeneo mengi yakiwa hayafikiki.

Meja Jenerali Ariel Bernardo, kamanda wa jeshi anasema watu dazeni mbili wamefanikiwa kuokolewa baada ya kuvutwa kutoka katika tope na wanapatiwa huduma katika hospitali.

Eneo la jimbo la Pwani ya Davao kumeripotiwa pia vifo vya watu 81 taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la maafa katika eneo hilo.

Maeneo mengi ambayo yameathirika bado hayaendeki kutokana na kutokuwepo kwa umeme , ukosefu wa mawasiliano huku njia kuu kama barabara na madaraja zikiwa zimeharibiwa vibaya.

Helkopta za uokoaji zinaendelea na shughuli za kuwatafuta watu waliokwama katika tope ingawa hali ya hewa bado si nzuri.

Maelefu ya watu wako katika makazi ya muda na mahitaji ya kibinadamu kama maji , chakula na nguo yanazidi kuhitajika. Shule zimefungwa na safari za ndege nazo zimeahirishwa hii leo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef