Kim, Trump waanza siku ya pili ya mazungumzo
28 Februari 2019Trump alisifu kile alisema ni "uhusiano maalum” alipokutana na Kim katika mji mkuu wa Vietnam Hanoi hapo jana na akasema kuwa ameridhiswha na kasi ya mazungumzo, licha ya kuwepo kwa ukosoaji kuwa hayasongi haraka iwezekanavyo.
Ikulu ya Marekani imesema viongozi hao wawili wanapanga kusaini "makubaliano ya pamoja” baada ya kufanya mazungumzo zaidi leo. Hata hivyo haikutoa maelezo yoyote kuhusu sherehe hiyo ya utiaji saini, ijapokuwa mazungumzo ya pande zote yamejumuisha uwezekano wa taarifa ya kisiasa ya kutangaza kumalizika kwa Vita Vya Korea vya mwaka wa 1950 – 53, ambayo baadhi ya wakosoaji wanasema bado mapema.
Maafisa Marekani na Korea Kaskazini wamesema Trump na Kim pia walijadili kwa sehemu hatua za kuondoa silaha za nyuklia, kama vile kuwaruhusu wakaguzi kushuhudia kuharibiwa kwa kinu cha nyuklia cha Korea Kaskazini cha Yongbyon.
Makubaliano ya Marekani huenda yakajumuisha kufunguliwa kwa ofisi za mawasiliano au kuruhusu miradi kati ya Korea mbili, lakini wakosoaji wanasema Trump anakabiliwa na hatari ya kupoteza kabisa uwezo wa kujiinua kama atalegeza sana Kamba na kwa haraka.
Mkutano wa kilele wa Hanoi ni wa pili kwa Trump na Kim tangu mkutano wa kwanza nchini Singapore mwezi Juni ambao ulikuwa wa maneno tu na sio hatua zozote thabiti na tangu hapo hakujawa na maendeleo yoyote muhimu yaliyopatikana.
Rais huyo wa Marekani hata hivyo alionekana kuwa mchangamfu na Kim hata wakati wakili wake wa zamani Michael Cohen akitoa ushahidi katika kikao cha bunge mjini Washington, akimuita Trump "mlaghai” ambaye alifahamu kabla kuhusu kutolewa kwa barua pepe zilizoibiwa ambazo zililenga kumdhuru mpinzani wake wa Democratic katika kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2016.
Huku akikabiliwa na shinikizo nyumbani kuhusu uchunguzi wa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani, Trump anatafuta kupata ushindi kwa kujaribu kuishawishi Korea Kaskazini kuwachana na silaha zake za nyuklia kwa kubadilishana na ahadi za Amani na maendeleo, lengo la seria ya kigeni ambalo liliwatatiza watangulizi wake kadhaa.
Trump na Kim walifanya mazungumzo ya ana kwa ana kabla ya hafla ya chakula cha jioni ambayo ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani Mike Pompeo, kaimu mkuu wa shughuli za serikali Mick Mulvaney, mjumbe mkuu wa Kim Yong Chol na Waziri wa Mambo ya kigeni wa Korea Kaskazini Ri Yong Ho.
Hii leo, viongozi hao wawili wana msururu wa mikutano kwenye hoteli ya Metropole, wakianza na mazungumzo mengine ya ana kwa ana ambayo yatadumu kwa dakika 45.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu