Kim Jong Un atoa wito wa kuimarishwa kwa jeshi la wanamaji
29 Agosti 2023Kiongozi wa Korea Kaskazini ameendelea kueleza kuwa, jeshi lake la wanamaji linahitaji kuwa macho na kuwa tayari kwa vita.
Katika hotuba ya kuadhimisha siku ya jeshi la wanamaji, Kim Jong Un amesema Marekani, Japan na Korea Kusini zilitangaza ushirikiano wa mara kwa mara wa kufanya luteka za kijeshi; kuashiria juu ya makubaliano walioafikiana kwenye mkutano wa kilele uliofanyika Agosti 18 katika jimbo la Maryland, Marekani.
Katika mkutano wa kwanza kati ya viongozi wa Marekani, Korea Kusini na Japan, walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi hasa wakati huu ambapo wanajaribu kupunguza ushawishi wa China unaoongezeka.
Wiki iliyopita, Korea Kusini na Marekani zilianza luteka za kijeshi kama jibu kwa vitisho vya nyuklia na makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini.
Pyongyang hata hivyo imeshutumu luteka hizo na kueleza kuwa ni mazoezi ya kujiandaa kwa vita.