Kila Mkenya aliyetimiza miaka 18 kulipia bima ya afya
30 Septemba 2021Huduma zitakazotolewa kwenye hospitali za umma ni pamoja na maradhi yasiyohitaji mgonjwa kulazwa na saratani au upasuaji. Bunge la taifa limepitisha kwa kauli moja kuwa kila Mkenya aliyetimiza umri wa miaka 18 anapaswa kulipia bima ya afya ya kitaifa. Hii inamaanisha kuwa kila aliye kwenye kundi hilo atalazimika kulipia shilingi 500 pesa za Kenya kwa mwezi au alfu 6 kwa mwaka kugharamia matibabu. Hayo yamesemwa na Peter Kamunyo Gathege, afisa mkuu mtendaji wa hazina ya kitaifa ya matibabu NHIF.
Huduma hizo za afya ni pamoja na matibabu ya magonjwa yasiohitaji kulazwa, uzazi, matatizo ya figo, saratani na upasuaji. Mabadiliko hayo ya sheria ya huduma za afya kwa umma ni sehemu ya mpango wa kutoa huduma za afya kwa kila mkenya, UHC.
Hata hivyo, wabunge hawakuyaunga mkono mapendekezo ya kamati ya bunge ya afya ya kitaifa yaliyotaka kuzishinikiza serikali kuu na za kaunti kugharamia huduma za matibabu kwa watu milioni 5.1 wasiojiweza.
Kwa upande mwengine, bodi ya hazina ya kitaifa ya matibabu, NHIF ndiyo itakayoamua kiwango watakachochangia watu wasiokuwa na ajira. Waajiri wa wafanyikazi wanaopokea mshahara chini ya shilingi alfu 12 watalazimika kuongezea mchango wao wa bima hiyo ya NHIF.
Kwa sasa watu wanaopokea mshahara wa kati ya shilingi alfu 8 na 11,999 wanachangia shilingi 400 kila mwezi. Kiasi cha juu zaidi cha kuchangia kwenye bima hiyo kwa wafanyakazi walioajiriwa ni shilingi 1,700. Kwa waliojiajiri, wabunge waliunda makundi matatu na viwango vya fedha watakazochangia kwenye bima hiyo ya NHIF. Takwimu rasmi zinaashiria kuwa wakenya milioni 25.36 wametimiza miaka 18. Kimsingi,mchango wa watu wote hao ungekiongeza kwa mara tatu kiasi cha fedha kwenye hazina ya kitaifa ya matibabu kwa shilingi milioni 16.36.