Kikosi kwa ajili ya Mali, chaidhinishwa
26 Aprili 2013Azimio hilo lililopitishwa jana Alhamisi mjini New York, Marekani, linaidhinisha hatua ya kupeleka nchini Mali wanajeshi 12,600 mwezi Julai mwaka huu, kikosi ambacho kitachukua nafasi ya majeshi ya Ufaransa na yale ya Afrika ambayo yanapambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika kikosi hicho, kutakuwa na wanajeshi 11,200 na polisi wa kimataifa 1,440, wengi wao wakiwa wanatoka kwenye kikosi cha wanajeshi 6,300 kutoka mataifa 10 ya Afrika, ambao tayari wako Mali.
Hata hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, litaamua iwapo mzozo wa Mali umepungua vya kutosha na kutokuwa na haja ya kukipeleka kikosi hicho, au kikosi hicho kikapelekwa mapema zaidi iwapo hali itazidi kuwa mbaya.
Kazi za kikosi kipya
Azimio hilo la Umoja wa Mataifa kifungu namba 2100 linaeleza kuwa, kikosi hicho kipya cha umoja huo kitakachojulikana kama MINUSMA, kinapaswa kutumia njia zote zinazowezekana kurejesha utulivu kwenye miji mikubwa, kuwalinda raia, kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Mali, pamoja na kuisaidia serikali ya Mali kuongeza mamlaka yake katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na vikosi vya kulinda amani vya Umoja huo, Herve Ladsous, amewaambia waandishi wa habari kuwa wanajua kutakuwa na mazingira tete. Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kitachukua nafasi ya kikosi cha wanajeshi 6,000 kinachoongozwa na Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amepongeza hatua ya kuidhinishwa kwa azimio hilo, akisema kuwa linathibitisha uungwaji mkono wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa katika hali ya kuleta utulivu kaskazini mwa Mali, pamoja na hatua ya Ufaransa kuivamia kijeshi nchi hiyo.
Kikosi cha Ufaransa kuiunga mkono MINUSMA
Hata hivyo, Ufaransa imeanza kuondoa wanajeshi wake nchini Mali wapatao 4,500, lakini itawabakisha wanajeshi 1,000 kwa ajili ya kupambana na waasi. Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema kuwa wanajeshi wake watakaobakia Mali, watakuwa tayari kutoa msaada kwa kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa iwapo itahitajika.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Tiemen Hubert Coulibaly, amesema kuwa kuidhinishwa kwa azimio hilo ni hatua muhimu kusaidia kumaliza mzizi wa shughuli za magaidi na makundi yenye silaha. Aidha amesema hatua hiyo inasaidia kuimarisha mazungumzo na upatanishi baina ya wananachi wa Mali na kuhakikisha kuwa amani inakuwepo kuzunguka nchi nzima.
Majeshi ya Ufaransa yaliingia Mali mwezi Januari mwaka huu, baada ya serikali kuomba msaada wa kuwazuia waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kuingia kwenye mji mkuu wa Bamako.Majeshi ya Ufaransa na Chad yalifanikiwa kuwaondoa waasi kutoka kwenye miji ya kaskazini mwa Mali.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef