220711 Äthiopien Hunger
25 Julai 2011Wajumbe wa serikali, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa mashirika ya misaada leo wanakutana mjini Rome kwa ajili ya kikao cha dharura kulijadili baa la njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika. Wajumbe kwenye kikao hicho wanazungumzia njia za kuwasaidia watu wapatao milioni 12 waliomo katika hatari ya kufa njaa.
Kikao hicho kinafanyika kufuatia shinikizo la kimataifa kuwataka viongozi wa dunia waongeze misaada kwa ajili ya mamilioni ya watu wanaotishiwa na baa la njaa lilisosababishwa na ukame mbaya ambao haujawahi kuonekana katika historia ya miaka 60 iliyopita katika eneo la Pembe ya Afrika.
Vifo vimekuwa vingi
Kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa Umoja wa Mataifa njaa imeshawaua maalfu ya watu katika sehemu hiyo .
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban - Kimoon ametoa mwito kwa wafadhili wa kuchangisha kiasi cha dola Bilioni 1.6 kwa ajili ya sehemu mbili za kusini mwa Somalia zilizotangazwa na Umoja wa Mataifa wiki iliyopita kuwa sehemu zenye maafa ya njaa.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa lililouandaa mkutano huo wa mjini Rome leo limetahadharisha kwamba hali itazidi kuwa ya maafa makubwa ikiwa hatua hazitachukuliwa.
Nchi zilizokumbwa na athari za ukame kwenye pembe ya Afrika ni pamoja na Kenya, Uganda,Sudan, Djibouti na Ethiopia.
Mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos ameitembelea Somalia na kujionea mwenyewe jinsi hali ilivyo.
Akizungumza na waandishi habari mjini Addis Ababa alieleza kuwa,
"Sasa hivi natokea kwenye jimbo la Somalia.Huko niliweza kuzungumza na wanawake waliotembea pamoja na watoto wao kwa muda wa saa tano wakitafuta chakula na huduma za afya.Watoto zaidi na zaidi wanasibika na utapiamlo. Wafugaji wameipoteza mifugo yao na hivyo wamepoteza njia za kujiendeshea maisha."
Utapia mlo na njaa
Nchini Ethiopia watu milioni nane yaani asilimia 10 ya wananchi wanasibika na utapiamlo. Licha ya juhudi za serikali ya Ehtiopia kuongeza vitega uchumi katika sekta ya kilimo bado hali haijawa nzuri sana. Pamoja na hayo sera ya kuwakodisha ardhi wakulima kutoka nje ya nchi inazidi kukosolewa.Kutokana an hali hiyo Ethiopia inayojiita kuwa chui milia wa Afrika bado inaandamwa na gamba la njaa.
Mwaka jana Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi alisema miongoni mwa malengo ya mpango wa maendeleo wa maika mitano ni kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula sambamba na kuzalisha cha ziada kwa ajili ya kuuza nchi za nje. Lakini hali halisi ni nyingine kwa Ethiopia mnamo mwezi wa februari WaziriMkuu Zenawi alilazimika kuomba msaada wa chakula kutoka kwa shirika la chakula duniani WFP kwa ajili ya wananchi wake milioni tatu waliokuwa wanatishiwa na njaa .
Mwandishi/Schadomsky ,Ludger - Mtullya Abdu
Mhariri/ Abdul-Rahman, Mohamed