Kijiji cha Kogelo changoja kuwasili kwa Obama
21 Julai 2015Baba yake Obama alikulia katika kijiji cha Kagelo, kabla ya kusafiri kwa masomo kwenda Marekani. Huko alikutana na kuoana na mama yake Obama, Ann Dunham, na kuwa mke wake wa pili kati ya wake wanne alioowa katika maisha yake na kuzaa nao watoto kadhaa.
Hata hivyo, wawili hao walitengana baada ya muda mfupi, na baba huyo alijiondoa katika maisha ya Obama na mama yake. Lakini mwaka 1982, baada ya baba yake Obama kupata ajali ya gari mjini Nairobi na kufariki, Obama aliamua kuitembelea Kenya kwa mara ya kwanza kulitafuta chimbuko lake kwa upande wa baba. Huko Obama alikutana na jamaa zake kadhaa, na safari hii inahadithiwa kwa upana katika kitabu cha wasifu wake "Dreams From My Father" kwa maana ya "Ndoto Kutoka Kwa Baba Yangu."
Said Obama, baba mdogo wa Rais Barack Obama na ambaye bado anaishi katika kijiji chao cha Kogelo, ni mtoto wa babu yake Rais Obama, Hussein Onyango, aliyemzaa na bibi yake wa kambo, Mama Sarah. Anasimulia ziara ya mtoto wake huyo Kenya ya mwaka 1987.
"Barack alikuwa akija hapa kijijini kututembelea na hamna aliyekuwa akishughulika. Tukienda mjini Nairobi na tukipanda magari ya matatu, tukitembelea mitaa ya mabanda, na hamna aliyekuwa akimshangaa. Lakini baada ya Obama kuingia katika siasa, maisha yake na ya familia yake yakawa yanaandamwa na dunia."
Said anaendelea kusema kuwa kijiji cha Kogelo awali kilikuwa hakijulikani lakini baada ya Obama kuwa rais wa Marekani sasa kimepata umaarufu.
Ziara ya Obama ya mwaka 2006 akiwa bado Seneta wa Marekani ilikuwa kama sarakasi. Ushindi wake wa urais wa mara zote mbili ulisheherekewa kwa vishindo nchini Kenya, na ziara yake nchini humo mwishoni mwa wiki inatarajiwa kusheherekewa kwa vishindo zaidi, huku Wakenya wakijisahau Obama sio Mkenya bali ni Mmarekani.
'Obama kama bidhaa'
Hii ni hata kwa wafanyabiashara ndogondogo. Hosea Owuor anayefanya biashara katika soko la Kisumu barabara ya Achieng Oneko anasema kwa mtazamo wa kibiashara "Obama ni kama bidhaa."
Owuor anategemea kutengeneza faida kupitia ziara ya Obama ya mwezi huu. Tayari ameshaagiza tisheti 400 zenye chapa ya sura ya Obama akitabasamu. Kawaida Owuor anauza nguo za mitumba na bidhaa za plastiki za Kichina, lakini anasema ziara ya Obama imempa mtindo mpya wa biashara. Kijana huyu pia anaamini kuwa Obama alizaliwa Kaunti ya Siaya, kilipo kijiji cha Kogelo, ingawa ukweli wa mambo ni kuwa rais huyo wa Marekani alizaliwa katika visiwa vya Hawaii.
Kijijini kwenyewe Kogelo, Manasseh Oyucho, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Seneta Obama, kwa faraja anamtambua Obama kama "Mkenya", "Mluo" na "Mkogelo", kama kwamba Obama alizaliwa katika kijiji hicho cha watu 3,000 kilichozungukwa na milima.
Kama watu wengine wengi katika kijiji cha Kogelo, mwalimu mkuu huyo wa miaka 56 anamshukuru rais Obama kwa mabadiliko mengi yaliyotikea katika siku za karibuni ndani ya kijiji hicho.
"Obama alipoingia madarakani ndipo kijiji cha Kogelo kilipojengewa barabara ya lami, na kupatiwa maji safi ya kunywa. Pia ndipo shule hii ilipojengwa, pamoja na kituo cha polisi. Yote haya yamekuja baada ya Obama kuwa rais," anasema Oyucho.
Umeme wa gridi kwa mara ya kwanza ulifika kijijini huko masaa machache baada ya Obama kushinda urais mwaka 2008.
Obama 'Mjaluo'
Sarah Obama, bibi yake Rais Obama wa kambo na mwenye umri wa miaka 94, anasema yeye ndiye kiongozi ya familia ya Obama. Kwa Wakenya anajulikana kama Mama Sarah lakini ni bibi kwa Rais Obama.
Mama Sarah anasema Rais Obama anajifundisha kiluo ambayo ndio lugha ya kabila lao. "Nitamsalimia na atanijibu katika lugha yetu ambayo tayari anaijua. Ataniuliza: 'Indhi nade, dani?" - inayomaanisha 'Hali yako bibi?' "Na mimi nitamjibu: 'Adhi maber, nyakwara," yenye maana 'Sijambo, mjukuu wangu.'
Kwa Wakenya wengi, Rais Obama ni mtu anayewapa msukumo. Alichowaonesha ni kwamba licha ya kuwa ametoka katika familia isiyokuwa ya kitajiri, lakini ameweza kuinuka na kuwa mmoja ya watu wenye nguvu kabisa duniani.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef