1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Scalia chatikisa kinyang'anyiro cha urais Marekani

15 Februari 2016

Kifo cha ghafla cha Jaji Antonin Scalia, kigogo wa kihafidhina katika Mahakama ya juu kabisaa ya Marekani, kimezusha mapambano makali katika mwaka huu wa uchaguzi kuhusiana na mrithi wake na mustakabali wa Marekani

https://p.dw.com/p/1HvUS
USA Jurist Antonin Scalia in Washington
Picha: picture alliance/ZUMA Press

Jaji Antonin Scalia alifariki dunia kutokana na mshutuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 79, na kuiwacha mahakama iliyokuwa imetawaliwa na wahafidhina, ikiwa na uwiano katika mwaka ambao umekuwa na kesi muhimu kuhusu utoaji mimba, utetezi wa walio wachache, uhamiaji na sheria ya mpango wa Rais Barack Obama kuhusu huduma za afya.

Habari hizo zilisababisha mawimbi katika kinyang'anyiro cha kuingia Ikulu ya White House, wakati wagombea wa Republican na Democratic wakielezea athari za kifo hicho cha ghafla. Katika ujumbe wake wa kwanza uliotikisa kinyang'anyiro cha kumrithi, saa chache tu baada ya kifo cha Scalia, Obama alisema atatekeleza majukumu yake ya kikatiba na kumteua mrithi.

USA Gedenken an Jurist Antonin Scalia in Washington
Bendera zilipepea nusu mlingoti MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Reynolds

Ikulu ya White House imesema kuwa rais Obama atasubiri hadi Baraza la Seneti litaporejea kutoka likizoni mnamo Februari 22 ndipo amteue mrithi wa Scalia.

Wagombea wakuu wa Republican – wakiwemo wagombea wote sita wa kihafidhina katika kinyang'anyiro cha urais – walitishia kuzuia uteuzi wowote utakaowasilishwa na Obama, wakihoji kuwa jukumu linapaswa kuachiwa rais ajaye kumteua atakayelijaza pengo la Scalia. Warepublican wanasema hakuna rais katika historia ya karibuni aliyemteua Jaji wa Mahakama Kuu kabisa katika mwaka wake wa mwisho madarakani.

Lakini Jaji Anthony Kennedy, aliyeteuliwa na Ronald Reagan, alithibitishwa mnamo mwaka wa 1988, ukiwa mwaka wa uchaguzi. Rais huwateuwa majaji wa Mahakama ya juu kabisaa, lakini baraza la Seneti linapaswa kuwaidhinisha kabla ya kuchukua usukani huo wa kudumu, wadhifa wa muda mrefu ambao huwawezesha wanachama wa mahakama hiyo kuepukana na shinikizo za kisiasa za kugombea madarakani..

Obama aliamuru bendera kupeperushwa nusu mlingoti kote Marekani baada ya kifo cha Scalia, huku akimsifu kwa kuwa “mmoja wa vigogo wa nyakati zetu”. Scalia alifariki dunia akiwa katika mbuga ya kibinafsi ya eneo la Big Bend magharibi mwa Texas, wakati akiwa katika safari ya uwindaji. Aliteuliwa katika Mahakama Kuu zaidi na Rais Ronald Reagan mwaka wa 1986.

Athari ya kifo chake kwenye mahakama hiyo itaoenekana maramoja, hata ingawa mapambano ya kumtafuta mrithi wake yataendelea kwa muda. Ikiwa na wafadhina 5 dhidi ya waliberali wanne, mahakama hiyo katika wakati wa karibuni ilikwamisha juhudi muhimu za utawala wa Obama kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na uhamiaji. Sasa wakati ikiwa imegawanyika nusu kwa nusu, 4-4, hukumu za mahakama ya chini zitadumishwa katika kesi ambazo zitaisha kwa uamuzi utakaogawa nusu kwa nusu hao majaji, na hivyo kuufanya udhibiti wa wahafidhina kuwa butu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga