Kifo cha rais Ghana chaweza kuleta mshikamano wa kitaifa
27 Julai 2012Hali ya mapambano miongoni mwa vyama imekuwa hulka inayofahamika katika nchi hiyo. Lakini baada ya kifo cha marehemu John Atta Mills mapambano yanaweza kupungua. Hayo kwa maoni ya wataalam ni hadithi ya mafanikio kwa sababu nchi za bara la Afrika zimekumbwa na vurugu nyingi katika kipindi cha mpito. Mkurugenzi mkuu katika almashauri inayoshughulika na utawala wa kidemokrasia nchini Ghana, Emmanuel Akwetey, alitaja nchi za Rwanda, Malawi na Nigeria ambayo awali zilikabiliwa na machafuko.
Aliongeza kuwa kwa nchi ambayo imekabiliana na misukosuko na kufanya majeshi yashike hatamu ya uongozi, hakupaswi hata kidogo kuachwa bila kiongozi. Aidha, makamu wa rais, John Dramani Mahama aliapishwa kama makamu wa rais masaa chache tu baada ya kutangazwa rasmi kwa kifo cha rais.
Awali raia walikuwa na maswali vichwani mwao juu ya nani atasimama kwenye uchaguzi mwezi Desemba kufuatia kifo cha John Atta Mills. Lakini sasa chama cha NDC tayari kimetangaza kuwa John Dramani Mahama ndiye atagombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala. Hatua ambayo ilionekana kuwa itaimarisha nafasi yake katika kugombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi ujao.
Naibu Katibu Mkuu wa NDC George Lawson, aliambia shirika la habari la Reuters kuwa hakukuwa na upinzani wowote kwenye maamuzi hayo na chama hicho kina imani kwa Dramani. Hali hii imeondoa mianya ya kuwepo mivutano na mitafaruku ndani ya chama kuhusu nani awe mgombea wakati huu wa kulelekea uchaguzi.
Bombaney, akizungumza na shirika la habari la IPS, alisema kuwa kufuzu kwa Ghana katika kipindi hicho cha mpito kumetokana kwa ukubwa na taasisi zake imara. Aliongeza kwamba ana imani Ghana itaendelea kuwa na uchaguzi wa amani mwezi Desemba.
Akwetey alisema pia kuwa raia wa Ghana wamepevuka na wamejifunza kutokana na mapambano ambayo wamekumbana nayo awali kwa mfano uongozi wa kimabavu. Kwa hivyo Ghana imeonyesha dunia kwamba inachukulia katiba yake kama kitu cha maana.
Kofi Owusu ,mwandishi wa habari aliyetuzwa na Msimamizi katika kituo cha redio cha Ultimate mjini Kumasi , alieleza hali ya kisiasa kabla ya kifo cha marehemu Mills kama yenye ukali. Wakati huo, watu walikuwa wakifikiria tu kuhusu atakayeshinda uchaguzi huo ujao.
Lakini Bombaney amesema kuwa Ghana kumpoteza rais wake itakuwa kama kumbusho kwa wananchi juu ya utambulisho wao wa aina moja na kuzuia vyama pinzani kurudi katika makabiliano makali ya awali .
Owusu pia aliambia IPS kuwa tayari viongozi wengine wameanza kuitazama msiba huo kama fursa ya kuimarisha umoja wa kitaifa.
Bombandey amesema, wabunge tayari wameonyesha kwa ukubwa hali ya umoja. Kila chama kimeonyesha mshikamano na serikali na pia familia inayoomboleza. Kwa maoni yake, kuanzia sasa, kutakuwa na mazungumzo ya kiheshima baina ya vyama pinzani ambayo pia itawezesha mazungumzo mazuri zaidi kuhusu mambo yenye umuhimu kwa nchi.
Mwandishi: Trizer Ochieng/IPS
Mhariri: Sudi Mnette