Kifo cha Rabbani ni pigo kwa amani Afghanistan
21 Septemba 2011Kifo cha Rabbani aliekuwa akiongoza jitahada za amani nchini Afghanistan, kimezusha wasiwasi mpya huku wengine wakiuliza iwapo nchi hiyo itarejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Bila shaka kifo hicho ni pigo kubwa kwa jitahada za kupatana na waasi nchini Afghanistan. Kwani yeye, alikuwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Amani linaloongoza jitahada za kujadiliana na Wataliban. Hiyo jana, Rabbani aliekuwa na miaka 71, alipanga kukutana na wanachama wawili wa Taliban nyumbani kwake. Mwanachama wa baraza hilo la amani, Fazel Karim Aymaq amesema, wageni wawili waliodai kuwa na ujumbe muhimu kutoka kwa Wataliban, walikaribishwa ndani ya nyumba. Mmoja wao alimkumbatia Rabbani na akaripua miripuko iliyofichwa ndani ya kilemba chake. Viongozi wa kimataifa wamelaani vikali mauaji hayo. Rais wa Marekani Barack Obama amesema:
"Tumepokea habari za huzuni hii leo kuwa rais wa zamani Rabbani aliekuwa akiongoza mchakato wa upatanisho ameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga. Alikuwa mtu aliejitolea kwa Afghanistan na alithaminiwa kama mshauri wa Rais Karzai. Vile vile ametoa mchango mkubwa kuijenga upya nchi. Kwa hivyo ni msiba mkubwa."
Na Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai aliekwenda Marekani kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ameamua kurejea nyumbani. Alipozungumza kwenye mkutano wake na Rais Obama, pembezoni mwa mikutano ya Umoja wa Mataifa, alisema ni siku ya uchungu mkubwa lakini pia ni siku ya umoja na ya kuendeleza jitahada za amani. Amesema, itakuwa shida kuziba pengo aliloliacha. Akaongezea:
„Ameyatoa mhanga maisha yake kwa ajili ya Afghanistan na amani ya nchi. Alijibebesha jukumu lililo muhimu kwa watu wa Afghanistan na usalama wa taifa na amani nchini mwetu."
Hata kama hakuna uhakika iwapo Rabbani, angefanikiwa kupata makubaliano ya amani katika nchi iliyokumbwa na vita vya miongo mitatu, moja ni hakika: mauaji yake ni pigo kwa jitahada za serikali na yamedhihirisha jinsi waasi walivyojiimarisha. Vile vile, kifo cha Rabbani wa kabila la Tajik, huenda kikatifua zaidi uhusiano wenye utata, kati ya makundi ya kikabila ya walio wachache na jamii kubwa ya kabila la Pashtun nchini Afghanistan.
Leo mjini Kabul, mamia ya watu waliobeba picha za Rabbani na mabango wamekusanyika karibu na nyumba yake kumkumbuka mwanasiasa huyo na kupinga mauaji yake. Wengine wamekusanyika nje ya mlango mkuu wa nyumba ya Rabbani wakisoma Qurani. Rais Karzai amesema, Rabbani atazikwa keshi au kesho kutwa kwa heshima za taifa.
Mwandishi: Martin,Prema/ Hasrat-Nazimi, Waslat
Mhariri: Abdul-Rahman