1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khan azindua maandamano ya mwendo mrefu

28 Oktoba 2022

Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan, amezindua kile kinachoitwa "maandamano ya mwendo marefu" kudai uchaguzi wa mapema, hatua inayoongeza shinikizo kwa serikali ambayo tayari iko kwenye mzozo.

https://p.dw.com/p/4IoPv
Pakistan | Imran Khan
Picha: K.M. Chaudary/AP Photo/picture alliance

Khan ambaye pia alikuwa mchezaji wa kimataifa wa kriketi, aliondolewa madarakani mwezi Aprili kwa kura ya kutokuwa na imani naye baada ya kujiondoa kwa baadhi ya washirika wake wa serikali ya muungano, lakini bado anauungwaji mkono mkubwa wa umma nchini humo.

Maelfu ya watu watarajiwa kujiunga na maandamano

Maelfu ya watu wanatarajiwa kujiunga na msafara wake utakaosafiri karibu kilomita 380 kutoka mji wa Lahore hadi kwenye mji mkuu Islamabad wiki ijayo, na kusimama njiani kufanya mikutano na kukusanya waandamanaji zaidi.

Muhammad Mazhar, mwanamume wa umri wa maiaka 36 aliyewasili Lahore siku ya Ijumaa kushiriki katika maandamano hayo, amesema kuwa wanahitaji kuwaondoa "waporaji na wezi wanaochukuwa fedha za serikali kwa maslahi yao wenyewe."

Mazhar ameongeza kuwa wanahitaji "kuiokoa nchi hiyo na kubadili mfumo, hivyo basi anamuunga mkono Khan."

Usalama waimarishwa Islamabad

Usalama tayari umeimarishwa katika mji mkuu Islamabad, huku mamia ya makontena yakiwa yamewekwa kwenye maeneo ya makutano ya barabara muhimu, kuwazuia waandamanaji iwapo watajaribu kuvamia majengo ya serikali.

Maandamano hayo yanakuja wakati serikali tawala ya muungano nchini humo, inajikakamua kufufua uchumi unaoyumba na kukabiliana na athari za mafuriko mabaya yaliosababisha thuluthi moja ya nchi hiyo kufunikwa kwa maji na kusababisha gharama ya ukarabati ya takriban dola bilioni 30.

Sababu za kuondolewa madarakani kwa Khan

Khan alichaguliwa waziri mkuu mnamo mwaka 2018 katika misingi ya kupinga ufisadi na wapiga kura waliochoshwa na siasa za nasaba, lakini ushughulikiaji wake mbaya wa uchumi na kutofautiana na jeshi linaloshutumiwa kumsaidia kuinuka kisiasa, kulihitimisha utawala wake.

Pakistan Lahore Unabhängigkeitstag
Mkutano mkubwa wa Khan mjini LahorePicha: Tanvir Shahzad/DW

Mara kwa mara, Khan amelishtumu jeshi hilo kwa kujaribu kumtenga  na amekwepa changamoto nyingi za kisheria tangu kuondolewa kwake.

Idara za usalama zafanya mkutano na wanahabari

Siku ya Alhamisi, mkuu wa idara kuu ya kijasusi nchini humo na mkuu wa mahusiano ya umma wa jeshi, walifanya mkutano na wanahabari ambao haujawahi kushuhudiwa,  ambapo walitetea taasisi hizo dhidi ya tuhuma za Khan kuwa zinaingilia siasa.

Katika ujumbe kupitia video siku ya Alhamisi, Khan alisema kuwa haogopi chochote ikiwa ni pamoja na kukamatwa. Khan aliongeza kuwa watu wanataka kutimizwa tu kwa jukumu moja la serikali, uchaguzi huru na haki .

Serikali ya shirikisho nchini humo inayosimamia Islamabad, imesema kwamba ukiukaji wowote kutoka kwa mipango ya maandamano iliyoidhinishwa utakabiliwa kwa nguvu kutoka kwa polisi mjini humo.

Majimbo yanayopakana na Islamabad yatarajiwa kutoa ulinzi 

Chama cha Khan kiko serikalini katika majimbo mawili yanayopakana na Islamabad ya Punjab na Khyber- Pakhtunkwa na vikosi vya polisi katika majimbo hayo vinatarajiwa kutoa ulinzi kwa waandamanaji.

Huku usalama ukiwa umeimarishwa Islamabad na kuongezwa kwa vikosi vya kijeshi, kuna wasiwasi kwamba huenda vikosi vya pande hizo mbili vikakabiliana.