Khamenei alaani shambulizi katika ubalozi wa Saudi Arabia
20 Januari 2016Kiongozi huyo mwenye maamuzi ya mwisho nchini Iran amesema kama ilivyo kwa shambulizi dhidi ya ubalozi wa Uingereza lililotokea kabla, shambulizi kwenye ubalozi wa Saudi Arabia, lilikuwa kinyume na matakwa ya Iran na dini ya Kiislamu na hakupendezewa hata kidogo na kile kilichotokea. Ubalozi wa Uingereza ulivamiwa na kundi la watu mwaka 2011.
Hata hivyo shambulizi la hivi karibuni katika ubalozi wa Saudi Arabia, ambapo vyombo vya habari vimeripoti kukamatwa kwa watu 40 wanaodaiwa kuhusika, lilisababisha Riyadh mara moja kukatiza mahusiano ya kidiplomasia na Tehran. Tukio hilo la uvamizi lilitokea usiku baada ya Saudi Arabia kutekeleza adhabu ya kifo kwa kiongozi wa kidini wa madhehebu ya kishia Nimr al Nimr. Khamenei pamoja na maafisa wa Iran waliushambulia utawala wa Saudi Arabia kwa kutekeleza hukumu hiyo ya mauaji.
Lakini matamshi ya leo ya Khamenei ya kukemea tukio hilo aliyoyatoa mbele ya maafisa wa uchaguzi, kuelekea uchaguzi wa bunge tarehe 26 mwezi wa Februari, yameelezea wazi kuwa Iran haiwezi kubebeshwa mzigo wa shambulizi hilo. Kwa upande wake rais wa Iran Hassan Rouhani wakati huo alisema tukio hilo lilitekelezwa na wahalifu wanaochukua hatua dhidi ya matakwa ya nchi.
Aidha wahalifu hao walichukua picha na video ambapo walionekana wakishikilia bidhaa walizokuwa wameiba ndani ya ubalozi huo wa Saudi Arabia, jambo lililoitia aibu kubwa serikali ya Iran. Rais Rouhani na maafisa wengine wamelaani tukio hilo lililoonekana na mamilioni ya watu duniani kupitia mitandao ya kijamii. Rouhani sasa anataka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwashitaki waliyohusika.
Huku hayo yakiarifiwa pia Khamenei kwa mara ya kwanza amezungumzia hatua fupi iliyochukuliwa na kikosi cha mapinduzi Iran kuwashikilia mabaharia 10 wa Marekani waliyoingia katika maji ya Iran kimakosa katika bahari ya Guba. Khamenei amesema hatua iliyochukuliwa na kikosi hicho cha vijana dhidi ya maadui zao ni hatua ya kupongezwa.
"Sikupata nafasi ya kuwapongeza, nawapongeza kwa hatua waliyopaswa kuchukua," aliongeza Khamenei. Kukamatwa kwa mabaharia hao wa Marekani mnamo januari 13 kumekuja siku kadhaa kabla ya Iran kufikia tarehe yake ya kutekeleza mpango wa ke wa nyuklia na mataifa yaliyo na nguvu duniani ikiwemo Marekani.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga