1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Zuma yasikilizwa tena

19 Julai 2021

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amejitokeza leo kwa mara nyingine kwa njia ya video, wakati kesi ya ufisadi dhidi yake ilipoendelea kusikilizwa kwenye mahakama ya juu nchini humo.

https://p.dw.com/p/3whUj
Jacob Zuma | Korruptionsverfahren
Picha: Phill Magakoe/Reuters

Zuma amejitokeza hii leo (Jumatatu) kuiomba mahakama kusongezwa mbele kwa kesi hiyo. Kesi hii inaendelea baada ya zaidi ya wiki mbili tangu alipohukumiwa kifungo cha miezi 15 jela kwa kuidharau mahakama, hatua iliyochochea kuzuka ghasia katika baadhi ya maeneo nchini humo. 

Zuma akiwa amevalia suti nyeusi na tai nyekundu hakusema chochote, wakati mmoja wa mawakili wake Dali Mpofu alipokuwa akiIomba mahakama kuisogeza mbele kesi hiyo, ili kumruhusu Zuma kujitokeza mwenyewe, huku akipinga njia hiyo ya video.

Kituo cha televisheni cha nchini humo cha Newzroom Afrika kilionyesha magari yenye silaha yakiwa yameegeshwa nje ya jengo la mahakama. Kulishuhudiwa pia maafisa wa usalama wakiwa wamezungushia kizuizi jengo hilo hilo lililoko katika mji wa Pietermaritzburg, kusini mashariki mwa taifa hilo, na ambako ni mji mkuu wa jimbo la Kwa-Zulu Natal. Eneo hilo liliathirika pakubwa na ghasia hizo.

Hata hivyo, baada ya muda kizuizi hicho kiliondolewa ili kuruhusu watu kupita kwenye mtaa huo baada ya watu waliojitokeza kuondoka.

Wakili Mpofu amesema Zuma bado hajapata fursa nzuri ya kujadiliana na timu yake ya mawakili baada ya kujisalimisha mwenyewe mapema mwezi huu kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela kutokana na kosa hilo la kuidharau mahakama.

Südafrika Ex-Präsident Zuma tritt Haftstrafe an | Protest
Kulizuka ghasia kubwa nchini Afrika Kusini baada ya Zuma kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 jela na kusababisha uharibifu mkubwa.Picha: Rogan Ward/REUTERS

Wakili huyo ameiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa hadi wiki tatu, na kusema anaamini katika kipindi hicho tayari mahakama hiyo ya kikatiba itakuwa imefanya maamuzi kuhusiana na ombi la Zuma la kupitiwa upya kifungo hicho.  

Hisia bado ni mseto kuhusiana na kifungo cha miezi 15 jela.

Baadhi ya wakaazi waliozungumza na shirika la habari la Reuters katika eneo hilo la Pietermaritzburg ambako leo kulishuhudiwa utulivu wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na kesi hiyo ya Zuma.

Martin Mamabolo alisema "Ninavyojua, Zuma ni fisadi.  Kwa hivyo lazima abaki gerezani na achukuliwe kama wengine waliofungwa kwa ufisadi. Na Robert Montsu naye alisema "Nchi hii sio ya Zuma peke yake, ni yetu wote. Tuliwachagua kwa ajili ya hawa watu halafu leo wanaitafuna peke yao.

Kenneth Fisana alikuwa na maoni tofauti kidogo, akiomba Zuma aachiwe huru. "Hapana, nadhani sina mengi ya kusema, lakini ninachijua ni kwamba Zuma angeachiwa tu kwa sababu ni mzee".

Katika hatua nyingine mawakili wa Zuma wanashinikiza kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka wa serikali Billy Downer kujiengua kwenye jopo hilo. Mawakili hao wanadai kwamba Downer alivujisha taarifa kuhusu kesi hiyo kwenye vyombo vya habari, huku Downer mwenyewe akiwatuhumu kuwa hiyo ni moja ya mkakati wao wa kuchelewesha kesi hiyo, ingawa mawakili wa Zuma wanapinga vikali.

Zuma anakabiliwa na makosa 16 ya ufisadi na matumizi mabaya ya mali ya umma. Anatuhumiwa kwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni ya kuuza silaha ya nchini Ufaransa ya Thales, katika mikataba tata ya manunuzi ya silaha ya mwaka 1999, ingawa kwa pamoja wanakana madai hayo.

Mashirika: AFPE/APE/RTRE