1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Pistorius kusikilizwa Machi mwakani

Elizabeth Shoo19 Agosti 2013

Mahakama mjini Pretoria imeamua kwamba kesi ya mwanariadha Oscar Pistorius itaanza kusikilizwa Machi 3 mwaka kesho. Pistorius, mwenye ulemavu wa miguu, ameshtakiwa kwa shutuma za kumuuwa mpenzi wake kwa risasi.

https://p.dw.com/p/19S4E
Oscar Pistorius mahakamani
Oscar Pistorius mahakamaniPicha: Getty Images/AFP/Stepahne De Sakutin

Msururu wa waandishi wa habari ulikuwa umejikusanya mbele ya mahakama ya mjini Pretoria. Wote walikuwa wanamsubiri Oscar Pistorius, mwanariadha aliyeng'ara katika michezo ya Olimpiki ya walemavu iliyofanyika mwaka jana jijini London, Uingereza.

Akiwa na uso wenye huzuni, Pistorius mwenye umri wa miaka 26, aliingia kortini akiwa amevaa suti nyeusi. Alisindikizwa na ndugu zake wawili, na kabla ya jaji kuanza kuzungumza, walishikana mikono wakilia na kusali.

Pistorius ameshtakiwa kwa kosa la kumuuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp, tukio lililotokea katika Siku ya Wapendanao mwaka huu. Maiti ya Steenkamp ilikutwa katika bafu la nyumba ya Pistorius ikiwa na imepigwa risasi kichwani, mkononi na pajani. Mashtaka mengine yanahusisha umiliki wa risasi kinyume cha sheria. Mahakama imeamua kwamba kesi ya Pistorius itaanza kusikilizwa rasmi tarehe 3 Machi mwakani.

Pistorius katika michezo ya Olimpiki ya London 2012
Pistorius katika michezo ya Olimpiki ya London 2012Picha: picture-alliance/AP

Pistorius kupewa kifungo cha maisha?

Pistorius amekanusha mashtaka yote na kwa sasa yuko nje kwa dhamana. Mwanariadha huyo ameeleza kwamba hakukusudia kumuuwa mpenzi wake, lakini aliposikia kuwa kuna mtu bafuni kwake alihisi kuwa labda ni jambazi na ndio maana akaanza kufyatua risasi.

Iwapo atakutwa na hatia, anaweza kupewa kifungo cha maisha. Kifungo cha chini kabisa kwa mtu aliyekutwa na kosa la kuuwa ni miaka 25. Afrika ya Kusini haina adhabu ya kifo. Kesi ya Pistorius itasikilizwa katika Mahakama Kuu ya Pretoria ambapo jaji mmoja ndiye atakayeamua iwapo ana hatia au la.

Polisi wakusanya ushahidi wa kutosha

Kwa kuwa upande wa mwendesha mashtaka unajaribu kumwonyesha Pistorius kama mtu mwenye hasira na anayependa kutumia silaha, inawezekana kuwa akashtakiwa kwa makosa mengine mawili yanayohisusha matumizi ya silaha.

Pistorius ameshtakiwa kwa kosa la kumuuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp
Pistorius ameshtakiwa kwa kosa la kumuuwa mpenzi wake Reeva SteenkampPicha: picture-alliance/AP

Mwanzoni mwa mwaka huu iliripotiwa kwamba Pistorius alionyesha bunduki hadharani alipokuwa katika mgahawa mmoja jijini Johannesburg. Katika kisa kingine alifyatua risasi kupitia dirisha la juu la gari la mpenzi wake wa wakati huo. Taarifa ya ofisi ya kamishna mkuu wa polisi wa Afrika ya Kusini, imesema kuwa wapelelezi, wataalamu wa silaha, teknolojia na wanasaikolojia wameshirikiana kutafuta ushahidi wa kumbana Pistorius na wameeleza kuwa wana uhakika kwamba ushahidi huo utatosha kumfanya mwanariadha huyo atiwe hatiani.

Iwapo Reeva Steenkamp bado angekuwa hai, leo angetimiza miaka 30.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri: Mohammed Khelef