1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya mashambulio ya treni ya Madrid

P.Martin14 Februari 2007

Kesi ya watu 29 wanaoshukiwa kuhusika na mashambulio ya bomu yaliofanywa dhidi ya treni mjini Madrid mwaka 2004,inafunguliwa leo hii.

https://p.dw.com/p/CHK8

Miongoni mwa washtakiwa hao,7 watakabiliwa na kifungo cha kama miaka 40,000 ikiwa watakutikana na hatia.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka,washtakiwa sita wametambuliwa kuwa ni waandalizi wakuu wa shambulio hilo la kigaidi ambalo ni baya kabisa kupata kutokea nchini Hispania.Watatu wanaoshukiwa kupanga njama ya kushambulia kwa bomu treni nne za abiria ni Rabei Ousmane Sayed Ahmed,Mmisri mwenye umri wa miaka 35 anaeshtakiwa kuua watu 191,kuhatarisha maisha ya wengine 1,824 na kuongoza kundi la kigaidi.Yeye anakabiliwa na kifungo cha miaka 38,656,lakini kuambatana na sheria ya Hispania anaweza kufungwa hadi miaka 40 tu.Mshtakiwa mwengine Hassan Al Haski au Abu Hamza ni Mmoroko mwenye miaka 43 na anakabiliwa na mashtaka na kifungo sawa na Sayed Ahmed.Yeye alikamtwa Desemba 21 mwaka 2004 kwa kushukiwa kuwa mwanachama wa Kundi la Kiislamu la Morocco- GICM-lenye mahusiano na Al-Qaeda na kuaminiwa kutoa fikra ya shambulio la Madrid.Wa tatu ni Yousef Belhadj,Mmoroko mwenye umri wa miaka 30 anaeshtakiwa kuwa ni mwaandalizi wa mikakti na yeye pia hukabiliwa na kifungo cha miaka 38,656.Yousef Belhadj aliekamatwa Februari mosi mwaka 2005 nchini Ubeligiji na kupelekwa Hispania ni binamu wa Mohamed Belhadj aliekodi fleti moja nje ya Madrid.Majuma matatu kufuatia mashambulio ya treni ya Madrid,watu saba walijiripua ndani ya fleti hiyo,polisi walipovamia jengo hilo la ghorofa.Mshtakiwa mwengine anakumbukwa na baadhi ya abiria wa treni,nae ni Mmoroko mwenye umri wa miaka 33,Jama Zougam.Yeye pia anashtakiwa kuhusika na mauaji ya watu 191,kuwajeruhi 1824 na kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi.Yeye alikamatwa Leganes amabalo ni eneo mojawapo la Madrid wanakoishi wageni wengi.Hapo awali jaji Baltasar Garzon anaepiga vita ugaidi,alionya kuwa Zougam ana mahusiano na kundi la tawi la Al-Qaeda nchini Hispania lililoshtakiwa kusaidia mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.Wakati huo Zougam hakushtakiwa.Hata Morocco iliiarifu Hispania kuwa Zougam ni mtu hatari.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa Hispania, mashambulio ya Machi mwaka 2004 mjini Madrid yalichochewa na mtandao wa Al-Qaeda wa Osama bin Laden.