Kesi ya kwanza ya Guantanamo chini ya Obama
11 Agosti 2010Habari zinazojulikana kuhusu yale yaliyotokea wakati wa kuwepo kizuizini ni kinyume na vigezo vya haki za binadamu za kimataifa na hiyo inazusha mashaka kuhusu ahadi za kuwepo uwazi zilizotolewa na Obama.
Obama aliahidi kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa jela ya Guantanamo itafungwa katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya serikali yake kuingia madarakani.Yeye ametaka uwepo uwazi na sheria kuheshimiwa katika mahakama ya kijeshi ya Guantanamo.Yajulikana kuwa ahadi ya kukifunga kituo hicho haikutimizwa na sasa hata ahadi zingine pia zipo hatarini.
Kweli yapo marekebisho yaliyofanywa na Obama,kwani wafungwa wanaofikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi ya Guantanamo, sasa wana haki zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa utawala wa Bush. Hata hivyo mahakama hiyo haitimizi vigezo vya kisheria, vya udemokrasia wa magharibi.Kwa mara ya kwanza tangu miongo kadhaa au hata tangu vita vikuu vya pili, nchi ya magharibi inamfikisha mfungwa mahakamani kwa mashataka ya uhalifu wa kivita unaosemekana kufanyika alipokuwa mtoto. Kwani Omar Khadr mwenye uraia wa Kanada, alikuwa na umri wa miaka 15 alipokamatwa nchini Afghanistan katika mwaka 2002, ikidaiwa kuwa yeye alirusha guruneti iliyomuuwa mwanajeshi wa Kimarekani.
Habari zinazojulikana kuhusu kukamatwa kwake na kuzuiliwa jela ni ukiukaji wa Mkataba wa Geneva na makubaliano ya kimataifa kuhusu ulinzi wa askari watoto - makubaliano yaliyotiwa saini na Marekani pia. Khadr alipohijiwa kwa mara ya kwanza, wala hakuwa na fahamu timamu kwani alikuwa amefanyiwa operesheni na alipewa dawa za kupunguza maumivu. Wakati wa mahojiano hayo, alionywa kuwa atabakwa au atauliwa ikiwa hatozungumza. Vile vile,aliteswa kwa kutoruhusiwa kulala. Huyo aliemhoji Khadr, baadae alishtakiwa kwa makosa ya kuwatesa wafungwa wengine.
Je,ushahidi unaopatikana kwa njia ya mateso una thamani gani? Ushahidi wa aina hiyo wala hautosikilizwa mbele ya mahakama ya kawaida. Lakini katika kituo cha Guantanamo, jaji moja wa kijeshi ameamua kuruhusu matamshi ya Khadr kutumiwa kama ushahidi. Na hiyo, licha ya Rais Obama kutangaza kuwa Marekani haitotumia tena matamshi ya kukiri makosa yanayopatikana kwa njia ya mateso. Wakati huo, Obama alipongezwa nyumbani na katika jumuiya ya kimataifa kwa hatua aliyoichukua.
Lakini habari za hivi karibuni kutoka Guantanamo zinasababisha wasiwasi kuhusu ahadi zilizotolewa na Obama. Uwazi ni tofauti kabisa na yale yanayotokea. Sasa ni dhahiri kuwa sio jela ya Guantanamo tu itakayoendelea kuwepo kwa muda fulani, bali hata utekelezaji wasiwasi wa kisheria uliokithiri huko.
Mwandishi: Müller,Sabine/ZPR
Mhariri: Othman,Miraji