1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Katanga kusikilizwa Kinshasa

3 Februari 2016

Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, leo imepanga kusikiliza kesi nyengine inayomkabili mbabe wa zamani wa kivita Germain Katanga , safari hii ikisikilizwa nyumbani.

https://p.dw.com/p/1HoVH
Niederlande Germain Katanga Internationaler Strafgerichtshof Den Haag
Picha: Michael Kooren/AFP/GettyImages

Itakumbukwa mwezi uliopita Gatanga alimaliza hukumu yake ya kifungo cha miaka 12 iliopitishwa na mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC mjini The Hague Machi 2014, kwa makosa ya uhalifu wa kivita, baada ya kukabidhiwa kwa mahakama hiyo.

Mnamo Januari 25 mwaka huu, mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ilimuamuru Germain Katanga kutoa maelezo yake ya kujitetea pamoja na orodha ya mashahidi wakati kesi itakaposikilizwa leo Februari 3.

Kesi hiyo inahusiana na mashtaka mapya ya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binaadamu yaliofunguliwa dhidi ya Katanga na mwendesha mashtaka mkuu wa jeshi mbele ya mahakama kuu ya kijeshi mjini Kinshasa.

Januari 21 Rais wa mahakama ya kimatifa ICC mjini The Hague aliwataka maafisa wa Congo kutoa maelezo ya ziada ili mahakama iamuwe ikiwa kuna haja ya kuruhusu kesi mpya dhidi ya mshtakiwa huyo, katika mahakama ya sheria nchini Congo.

Chini ya kifungu nambari 108 cha katiba ya ICC, nchi yoyote ambako mshitakiwa aliyehukumiwa na ICC anatumikia kifungo chake, inapaswa kuomba kibali kutoka mahakama hiyo ya kimataifa kabla ya kumfungulia mashtaka mapya. Katanga alirejeshwa Congo mnamo wiki za mwisho za kumaliza kifungo chake ili kumalizia kifungo hicho nyumbani.

HRW yataka kesi isikilizwe kwa kuzingatia haki

Mwanasheria na mkurugenzi katika Shirika la Haki za Binaadamu –Human Rights Watch Geraldine Mattioli-Zeltner, alisisitiza juu ya haja ya kesi dhidi ya Katanga kusikilizwa katika haki na sheria, akiongeza kwamba maafisa wa Congo wanapaswa kuipa mahakama ya ICC taarifa inazozihitaji, ili iweze kuamua ikiwa kesi mpya inaweza kufunguliwa.

Katanga amekuwa akimaliza adhabu aliyopitishiwa na ICC ya miaka 12 jela, katika gereza kuu mjini Kinshasa, baada ya kupatikana na hatia Machi 2014 kwa kuhusika katika uhalifu wa kivita katika kiji cha Bogoro wilayani Ituri.

Adhabu yake iliopunguzwa Novemba 2015 ilimalizika Januari 8 mwaka huu 2016, lakini Katanga akabakia gerezani kwa sababu ya mashtaka mapya nyumbani. Kesi iliosikilizwa na mahakama ya uhalifu ya kimataifa ilihusika tu na mauaji yaliotokea Bogoro.

Hii itakuwa ni kesi ya kwanza ambapo mashtaka mapya ya taifa yanawasilishwa dhidi ya mtu ambaye tayari alishashtakiwa na kuhukumi wa na mahakama ya ICC mjini The Hague.

Inazusha masuala muhimu juu ya mkakati wa uendeshaji mashtaka katika ICC na mafungamano kati ya mahakama hiyo na mahakama za kitaifa- katika kile kinachojulikana kama hatua zab ziada.

Shirika la Human Rights watch linasema, kesi hiyo itakuwa ni kipimo cha jinsi mfumo wa sheria nchini Congo unavyofanya kazi na uwezo wake wa kushughulikia yenyewe mashtaka mazito ya uhalifu wa kimataifa, katika utaratibu wa usawa na haki.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, HRW Press
Mhariri: Mohammed Khelef