1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi dhidi ya mtuhumiwa wa mauwaji ya halaiki ya wayahudi Demjanjuk yafunguliwe Munich

Oumilkher Hamidou30 Novemba 2009

Mtuhumiwa mkongwe Demjanjuk afikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwauwa maelfu ya wayahudi huko Sobibor

https://p.dw.com/p/Kkm7
Mtuhumiwa Demjanjuk afikishwa mahakamani kwa gari la wagonjwaPicha: picture-alliance / dpa

Kesi ya John Iwan Demjanjuk inaanza leo.Bwana huyo mwenye umri wa miaka 89 anatuhumiwa kusaidia katika visa 27.900 vya mauwaji-katika kambi ya maangamizi ya Sobibor,mashariki ya Poland. Kiroja ni kwamba Uzee na udhaifu wa mtuhumiwa haukusaidia kumuepushia kishindo cha kufikishwa mahakamani.Mzee mwengine pia,mtuhumiwa wa uhalifu wa vita, askari kanzu wa zamani wa wanazi-Heinrich Boere- anafikishwa pia mahakamani mjini Aachen.Kila miaka inapopita ,tangu vita vikuu vya pili viliporipuka ndipo nao wahalifu wanapozidi kuzeeka na kufariki.Suala linalozuka waliosalia ni wangapi?Na wangapi wanaweza kuhukumiwa.

Katika wakati ambapo Demjanjuk na Boere wanafikishwa mahakamani,wahalifu wengine bado wanaandamwa.Idara kuu inayoshughulikia visa vya uhalifu vilivyofanywa na wanazi,yenye makao yake Ludwigsburg karibu na Stuttgart ndiyo inayofuatilizia kesi hizo.Na shughuli za idara hiyo zinabidi kuendeshwa ipasavyo,la sivyo inakua shida kuwafungulia mashtaka wanaosakwa.

Katika kadhia ya Demjanjuk,ambae aliwahi kuhukumiwa na baadae kutokana na kutokuwepo uhakika kama ndio yeye,akabidi kuachiwa huru-safari hii lakini watumishi wa idara hiyo walitaka kuhakikisha kila kitu kinapita sawa na ushahidi dhidi ya Demjanjuk unapatikana- ndio maana wamelenga utafiti wao Sobibor-anasema Kurt Schrimm,mkuu wa idara hiyo mjini Ludwigsburg:

"Tumelenga shughuli zetu Sobibor,kwasababu Sobibor ilikua kambi ya maangamizi.Na kwa maoni yetu,kila mlinzi wa kambi hiyo alikua akijua nini kimetokea na kwa namna hiyo,amechangia pia katika kuuliwa watu hao."

Msaidizi wake,Joachim Riedel anasema katika kadhia ya Demjanjuk,kazi ilikua ngumu.Anasema wamefanya utafiki kwa muda wa miezi kadhaa na matokeo waliyoyapata wakayapeleka Munich.Muendesha mashtaka wa Munich akaendelea na uchunguzi wake,akawahoji kwa mfano watuhumiwa na mashahidi.

Vita baridi vilipomalizika fursa mpya ikajitokeza anasema Joachim Riedel

"Nilikwenda Ukraine mara nyingi na kusalia kwa muda mrefu.Niliweza kuingia katika maktaba ya serikali na kufungua madaftari na kufanikiwa kugundua kile nilichokua nikikitafuta.NImekwenda pia Moscow na kufungua maktaba ya idara ya upelelezi ya KGB.Na maktaba nyengine pia zilifuatia."

Prozess John Demjanjuk Montag 30.11.2009 Landgericht München
Jengo la mahakama mjini Munich inakosikilizwa kesi dhidi ya DemjanjukPicha: picture-alliance / dpa

Wahalifu 22 wakuu wa vita walihukumiwa katika korti maalum ya Nürnberg.Kesi nyengine 12 zikafuatia pia Nürnberg na nyengine kadhaa zikafunguliwa katika mahakama za kijeshi dhidi ya wahalifu wa utawala wa wanazi.Hatimae ndipo kesi zilipoanza kusikilizwa katika mahakama za makosa ya jinai.

Uchunguzi unaendelea mpaka hivi sasa nchini Ujerumani-dhidi ya watuhumiwa ambao majina yao yanawekwa siri.Wahalifu wangapi wa vita wamesalia,Joachjim Riedel anasema hawezi kukadiria.Hata hivyo wahalifu tangu wadogo wadogo mpaka wengine wakubwa wakubwa wametoroka.

Kwa vyovyote vile,Joachim Riedel anasema nawawe wazee vipi,watuhumiwa wakipatikana wanastahili kufikishwa mahakamani.

Mwandishi: Grathwohl,Daphne/ZR/Hamidou,Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman