1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry, Steinmeier wazungumzia ulinzi wa faragha

Admin.WagnerD28 Februari 2014

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ametumia ziara yake ya kwanza nchini Marekani tangu kufichuliwa kwa udukuzi wa Marekani nchini Ujerumani, kujadili ulinzi wa faragha na mwenzake John Kerry.

https://p.dw.com/p/1BHLQ
Mawaziri Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani na John Kerry wa Marekani katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Washington.
Mawaziri Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani na John Kerry wa Marekani katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Washington.Picha: Reuters

Wasiwasi uliibuka kati ya washirika hao mwaka uliopita baada ya nyaraka zilizovujishwa na wakala wa ujasusi wa Marekani Edward Snowden, kuonyesha kuwa shirika la usalama wa taifa la Marekani NSA, lilikusanya taarifa kuhusu raia wa Ujerumani na lilidukuwa mawasiliano ya simu ya mkononi ya Kansela Merkel na wanasiasa wengine wa Ujerumani. Waziri Kerry alisema baada ya chakula cha mchana na Steinmeier jana Alhamisi, kuwa mazungumzo baina yao yalikuwa ya tija. Steinmeier anatarajiwa kufanya mikutano zaidi kuhusu faragha na ujasusi leo mjini Washington.

Waziri Kerry alisema mataifa yao ni marafiki wa zamani na ni marafiki wa karibu, na kwamba wana uwezo wa kuzungumza kwa uwazi na kutafuta njia ya kushirikiana pamoja kuhusu masuala muhimu yanayowahusu wote. Yeye na Steinmeier walijadili hatua zaidi za kuimarisha ushirikiano wa kijasusi baina ya Marekani na Ujerumani, na kuongeza kuwa wataendeleza mazungumzo katika miezi ijayo.

Ufichuzi wa Edward Snowden uliathiri pakubwa uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani.
Ufichuzi wa Edward Snowden uliathiri pakubwa uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Walizungumza kwa kirefu juu ya uhusiano baina ya Washington na Berlin, ikiwemo namna ya kuweka urari kati ya usalama wa raia wao na faragha za raia hao. Ujerumani inataka kuwepo na mkataba wa kutochunguzana baina yake na Marekani lakini wito huo bado haujajibiwa mpaka sasa. Steinmeier anasema makubaliano kama hayo yangeboresha kwa kiasi kikubwa uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani, liliripoti jarida la habari la Ujerumani la Der Spiegel.

Ukraine yachomoza katika mazungumzo

Kerry alisema hali nchini Ukraine, ambako serikali mpya iko katika mchakato wa kuundwa baada ya miezi kadhaa ya machafuko, ilikuwa ya kipaumbele kwao, na ilichukuwa sehemu kubwa ya mjadala baina yake na Steinmeier wakati wa chakula cha mchana. Alimshukuru waziri Steinmeier kwa uongozi wake, akibainisha kuwa waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani alisafiri kwenda mjini Kiev na kusaidia kufikiwa makubaliano ya wiki iliyopita.

Hali nchini Ukraine ilikuwa miongoni mwa masuala yaliyozungumziwa na mawaziri Kerry na Steinmeier.
Hali nchini Ukraine ilikuwa miongoni mwa masuala yaliyozungumziwa na mawaziri Kerry na Steinmeier.Picha: Reuters

Ziara hii ya siku mbili ndiyo ya kwanza nchini Marekani tangu Steinmeier alipoteuliwa kuwa waziri wa mambo ya kigeni miezi miwili iliyopita. Alihudumu kama waziri wa mambo ya kigeni katika baraza la kwanza la Kansela Angela Merkel kuanzia mwaka 2005 hadi 2009.

Amekutana kwa mara kadhaa na waziri Kerry, ambaye alifanya ziara fupi mjini Berlin mwaka huu na kuhudhuria mkutano wa ulinzi na usalama mjini Munich. Akiwa mjini Washinton, Steinmeier anatarajiwa kukutana na John Podesta, mshauri wa juu wa rais Barack Obama, na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa, Susan Rice.

Steinmeier amepangiwa kuzungumzia hali ya ushirikiano kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani katika taasisi ya Brookings, katika hotuba inayotarajiwa kugusia mgogoro wa kisiasa nchini Ukraine na vita vya Syria. Kandoni mwa hayo, Steinmeier atakutana na mkuu wa shirika la fedha duniani, IMF, Christine Lagarde, kujadili hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili Ukraine.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Josephat Nyiro Charo