Kerry awasili Korea Kusini
12 Aprili 2013John Kerry ameanza ziara hiyo ya siku nne ya Asia Mashariki, itakayomfikisha hadi China na Japan, huku kukiwa na taarifa kwamba serikali ya Korea Kaskazini inaweza ikafyatua kombora la nyuklia Aprili 15 mwaka huu, lenye uwezo wa kuruka umbali mrefu hadi kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani katika pwani ya Guam.
Tarehe hiyo ni siku ambayo mwanzilishi wa taifa hilo, Kim Il Sung, alizaliwa. Katika ziara hiyo ya kwanza kuifanya Korea Kusini tangu ashike wadhfa huo, Kerry anatarajiwa kukutana na Rais Park Geun Hye na Waziri wa Mambo ya Nje, Yun Byung Se.
Kerry kutoa tamko
Maafisa wa Korea Kusini wamesema kuwa Kerry anatarajiwa kutoa tamko kuhusu Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikitoa vitisho dhidi ya Korea Kusini na Marekani. Ziara hiyo ya Kerry ina lengo la kuthibitisha ahadi ya Marekani kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi na Asia.
Ziara ya Kerry imefanyika wakati ambapo shirika la kijasusi la wizara ya ulinzi ya Marekani-DIA, ikitoa taarifa kuwa Korea Kaskazini inaweza kufyatua makombora yenye silaha za nyuklia.
Taarifa hizo zilielezwa jana Alhamisi wakati wa kikao cha kamati ya bunge ya huduma za kijeshi cha kuwasikiliza maafisa wa Pentagon kuhusu mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini. Hata hivyo, msemaji wa Pentagon, George Little, amesema haitakuwa sahihi kusema kuwa utawala wa Korea Kaskazini umeonyesha uwezo wake wa kufyatua kombora la nyuklia, ambao umetajwa katika ripoti hiyo.
Obama aitaka China kuishawishi Korea Kaskazini
Rais Barack Obama wa Marekani, ametoa wito wa kuwepo utulivu, huku akiisihi China kuishawishi Korea Kaskazini kuachana vitisho vyake na vitendo vya uchokozi. Rais Obama amesema hakuna mtu anayependa kuona ghasia au mizozo, lakini amesisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua zozote muhimu kuwalinda watu wake na washirika wake katika ukanda huo.
Hata hivyo, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Korea Kusini, Kim Min-Seok, amesema bado kuna shaka kama kweli Korea Kaskazini inaweza kutengeneza silaha za nyuklia zitakazokuwa na ukubwa wa kutosha kwenye makombora yake. Korea Kaskazini ambayo imedai Marekani inataka kuivamia, imetoa vitisho hivyo vya nyuklia, lakini wataalamu wengi wanasema kuwa Korea Kaskazini haiwezi kuanzisha mzozo ambao utaimaliza yenyewe.
G8 wailaani Korea Kaskazini
Ama kwa upande mwingine mwishoni mwa mkutano wao mjini London, Uingereza, mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani-G8, wamelaani vikali shughuli za nyuklia za Korea Kaskazini.
Mawaziri hao wameonya kuwa Korea Kaskazini inaweza ikakabiliwa na vikwazo vikali zaidi na kwamba nchi hiyo inaonyesha kukiuka moja kwa moja, maazimio manne ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aidha, wamesema wako tayari kuchukua hatua zaidi iwapo nchi hiyo itafanya jaribio jingine la kombora au nyuklia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFP,DPAE
Mhariri: Josephat Charo