Kerry atetea uvamizi wa Libya
7 Oktoba 2013Waziri John Kerry alisema kutekwa kwa Nazih Abdul-Hamed al-Ruqai, ambaye anadaiwa kuwa mwanachama wa kundi la Al-Qaeda mjini Tripoli mwishoni mwa wiki, kulifuata sheria za Marekani, na kufafanua kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa shabaha sahihi ya jeshi la Marekani, na kwamba atafikishwa mahakamani. Kerry alisema kuwa siyo muhimu kuwahurumia magaidi wanaotafutwa.
Al-Ruqai, ambaye anafahamika kwa jina lingine la Abu Anas al-Libi, alitekwa katika mitaa ya mji mkuu wa Libya Tripoli siku ya Jumamosi. Anatuhumiwa na Marekani kwa kushiriki katika mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani mjini Dar es Salaam na Nairobi mwaka 1998, ambayo yaliwaua watu zaidi ya 220.
Ametafutwa kwa miaka 12
Amekuwa katika orodha ya watu wanaotafutwa kwa udi na uvumba ya shirika la ujasusi la Marekani FBI, tangu orodha hiyo ilipoanzishwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, ambapo aliwekewa kitita cha dola za Marekani milioni 5 kwa atakaefanikisha kukamatwa kwake.
Kerry, ambaye ni mwendesha mashtaka wa zamani, alisema al-Libi ameshtakiwa na mahakama ya Marekani, na kwamba atapata fursa ya kujitetea.
Lakini waziri huyo wa mambo ya kigeni alikiri kuwa utawala mjini Washington haukutoa taarifa kwa serikali ya Libya kabla ya operesheni hiyo ya Jumamosi, na kuwaambia waandishi wa habari mjini Bali Indonesia, ambako anahudhuria mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi wa mataifa ya Asia na Pacific, kuwa Marekani inafanya kila lililo ndani ya mamlaka yake na lililo ndani ya mipaka ya sheria, kuwawinda magaidi.
"Ni mtu muhimu katika Al-Qaeda, na ni shabaha sahihi kwa jeshi la Marekani chini ya sheria inayoruhusu matumizi ya nguvu za kijeshi iliyopitishwa mwaka 2001," alisema Kerry.
Lakini aliongeza kuwa Washington haitoi taarifa makhsusi kwa serikali za kigeni, kuhusu operesheni kama hiyo iliyosababisha kutekwa kwa Libi. Serikali mjini Tripoli ilisisitiza kuwa uvamizi huo wa vikosi vya Marekani haukuidhinishwa rasmi, na chanzo cha karibu na Libi, kilisema kuwa alitekwa nyara wakati anarudi nyumbani kutoka Swala ya Alfajiri.
Operesheni ya Somalia yafeli
Siku ya Jumamosi, kikosi cha Delta Force cha jeshi la Marekani, ambacho kina jukumu la kupambana na ugaidi katika Afrika ya kaskazini, kilifanya mashambulizi pia nchini Somalia, ambapo waziri mkuu wa wake Abdi Farah Shirdon, alisema serikali yake ilishrikiana na Marekani katika operesheni hiyo, ambayo hata hivyo ufanisi wake haukubainika wazi.
Polisi ya Somalia ilisema watu saba waliuawa katika operesheni ya Barawe wakati jeshi la Marekani likisema lilisimamisha mapigano kuepuka kuwaua raia. Afisa ujasusi wa kisomali alisema kamanda mwenye asili ya Chechnya aliekuwa analengwa katika operesheni hiyo alijeruhiwa. Lakini msemaji wa Al-Shabaab Sheikh Abdiasis Abu Musab, alisema hakukuwa na kiongozi yeyote wakati wa shambulizi hilo, na kwamba wapiganaji wa kawaida walipambana kishujaa na kuwafukuza wavamizi.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, ape,afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.