Kerry: Afghanistan ipo pabaya
11 Julai 2014John Kerry amewasili katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul usiku wa manane akikabiliwa na kibarua kigumu cha kuutanzua mkwamo wa kisiasa katika nchi hiyo. Akizungumza katika ubalozi wa Marekani mjini humo ambao unao ulinzi mkali, Kerry alisema siasa za Afghanistan zimefika kwenye kona lenye hatari, na kuongeza kuwa uhalali wa matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi uko mashakani.
Kwa nyakati tofauti leo hii anatarajiwa kukutana na viongozi wawili waliopambana katika duru ya pili ya uchaguzi, Abdullah Abdullah na Ashraf Ghani, ambao kila mmoja wao anadai ndie mshindi atakayechukua nafasi ya rais anayeondoka madarakani, Hamid Karzai.
Kibarua kigumu huko mbele
Yeyote ambaye hatimaye atarithi wadhifa huo atakabiliwa na changamoto kubwa kuiongoza nchi hiyo iliyosambaratishwa na vita, baada ya vikosi vya kimataifa kuondoka, na kumuacha akikabiliana na kundi la wapiganaji sugu la Taliban.
Hata hivyo, waziri Kerry amesema ana matumaini kwamba itapatikana njia ya kujibu maswali yanayoulizwa, na kumaliza mashaka ya wananchi, na kuashiria mustakabali mwema wa Afghanistan. Pamoja na hayo lakini, Kerry ametoa tahadhari kwamba kwa sasa matumaini hayo sio kitu chenye uhakika.
Matokeo ya awali yameonyesha kuwa Ashraf Ghani anaongoza kwa wingi wa kura, lakini mpinzani wake, Abdullah Abdullah ambaye amewahi kabla kupoteza uchaguzi katika mazingira ya kutatanisha, amejitangaza mshindi, akidai amepokonywa ushindi kwa udanganyifu mkubwa.
Kambi ya Ashraf Ghani imeikaribisha ziara ya Kerry, ikisema ni hatua nzuri katika kutafuta suluhisho kwa mkwamo uliopo. Vile vile msemaji wa kambi ya Abdullah Abdullah amesema wanakaribisha juhudi zote zinazolenga kile alichokiita, ''kutenganisha kura safi na zile ambazo ni za udanganyifu''.
Maafisa wa Marekani wamesema Kerry atawashinikiza wagombea hao wawili kukubali ufanyike uchunguzi mkali juu ya namna zoezi la kupiga na kuhesabu kura lilivyoendeshwa.
Kitisho cha kukatiwa msaada
Waziri John Kerry amekutana kwanza na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Jan Kubis ambaye ameapa kwamba umoja huo utafanya kila kinachowezekana, kuhakikisha kwamba mchakato wa siasa za kipindi cha mpito unakamilishwa vyema, katika namna ambayo itaimilisha usalama na umoja nchini Afghanistan.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakutana kwa mazungumzo na rais Hamid Karzai, ambaye anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuiongoza nchi kwa miaka 13.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani amesema kwamba hakuna aliyetarajia uchaguzi usio na hitilafu kwa Afghanistan, bali Marekani imekuwa ikishinikiza kufanyika juhudi uchaguzi huo uwe na matokeo yanayoweza kukubaliwa na wote.
Marekani imezionya pande zinazozozana katika mgogoro huo wa baada ya uchaguzi, kwamba jaribio lolote la kuchukua madaraka kinyume cha katiba litaifanya nchi hiyo isitishe msaada wake kwa Afghanistan, ambao una thamani ya mabilioni ya dola kwa mwaka.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE
Mhariri:Josephat Charo