1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry aenda Misri na Doha

1 Agosti 2015

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ameondoka jana Ijumaa (31.07.2015) kwenda Misri kwa ajili ya mazungumzo ya ushirikiano na kisha atakwenda Qatar.

https://p.dw.com/p/1G8Fy
John Kerry stellt Bericht zum Menschenhandel vor
Waziri John Kerry wa MarekaniPicha: Reuters/G. Cameron

Akiwa nchini Qatar John Kerry anamatumaini ya kupunguza wasi wasi wa mataifa ya ghuba kuhusiana na makubaliano ya kinyuklia na Iran.

Ziara hiyo , ambayo itamalizika Agosti 8, haitajumuisha kwenda Israel, moja kati ya washirika wakubwa wa Marekani na mkosoaji mkubwa wa makubaliano mapya yaliyofikiwa ya kinyuklia.

Ägypten Pressekonferenz John Kerry und Sameh Shoukri 13.9.2014
John Kerry akiwa na Sameh Shoukri wa Misri walipokutana 13.09.2014.Picha: picture-alliance/dpa/K. Elfiqi

Wakati akiwa nchini Misri kesho Jumapili,(02.08.2015) Kerry atakutana na mwenzake Sameh Shoukri kwa ajili ya "majadiliano ya mkakati" kati ya washirika hao wa muda mrefu, ambao wamekuwa na uhusiano uliokumbwa na misukosuko mingi katika miaka ya hivi karibuni, kufuatia ghasia za kisiasa katika taifa hilo la Afrika kaskazini.

Mwishoni mwa mwezi Machi , Marekani iliondoa hatua yake ya kuzuwia msaada wa kila mwaka wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 1.3 kwa Misri.

Marekani yashutumu ukiukaji haki za biandamu

Lakini Marekani iliendelea na shutuma zake dhidi ya ukandamizaji wa kikatili wa utawala wa rais Abdel Fattah al-Sisi dhidi ya waungaji mkono wa mtangulizi wake , Mohammed Mursi.

Mdahalo baina ya maafisa hao wawili ni wa kwanza tangu mwaka 2009, na unakuja baada ya tangazo wiki hii kwamba Marekani imeanza kupeleka ndege za kivita chapa F-16 nchini Misri.

Pamoja na ushirikiano wa kijeshi, Kerry na Shukri watajadili "wasi wasi" wa Marekani kuhusu haki za binadamu.

USA Präsident Obama Treffen mit GCC Rat in Camp David
Rais Barack Obama alipokutana na wawakilishi wa mataifa ya baraza la Ghuba GCC, Camp DavidPicha: Reuters/K. Lamarque

"Tutajadili suala la mazingira ya kisiasa, suala la haki za binadamu wakati waziri akiwa mjini Cairo. Hii ni sehemu muhimu ya majadiliano ya kawaida," afisa wa wizara hiyo amesema.

Naibu waziri Tom Malinowski , atajiunga na Kerry , kwa mujibu wa afisa huyo, ambaye amesema "atakuwa na fursa ya kujadili pamoja na mwenzake baadhi ya masuala ambayo tunayo, baadhi ya wasi wasi ambayo tunao kuhusu hali hiyo."

Atakutana na mawaziri wa mataifa ya ghuba

Kerry atasafiri kwenda Doha siku ya jumatatu kukutana na wenzake kutoka mataifa wanachama wa baraza la ushirikiano katika mataifa ya ghuba (GCC).

Sababu kuu ya mkutano huo itakuwa ni kuondoa hofu waliyonayo kuhusu Iran, kufuatia makubaliano ya kinyuklia yaliyofikiwa Julai 14 mjini Vienna.

Nchi nyingi za ghuba zimesema zina wasi wasi juu ya nia ya Iran katika eneo hilo kufuatia makubaliano na Marekani pamoja na mataifa matano yenye nguvu duniani --Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi.

Saudi-Arabien Golf-Kooperationsrat in Riad
Picha: Fayez Nureldine/AFP/Getty Images

"Hii ni fursa, ya kweli , kwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani kupata kwa kina mawazo ya mawaziri wa mataifa ya ghuba GCC kujaribu kujibu maswali yoyote yaliyobaki ambayo wanayo na anamatumaini ya kuwaridhisha na kuhakikisha kwamba wanaunga mkono juhudi zetu za kusonga mbele," afisa huyo amesema.

Ameongeza kuwa mzozo nchini Yemen na Syria pia itajadiliwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri : Sudi Mnette