Kenyatta: Wanajeshi wa Kenya kuendelea na operesheni Somalia
15 Oktoba 2018Idara za Usalama nchini Kenya zimetakiwa kuwa macho katika mpaka wa Kenya na Somalia kwani wanamgambo wa Al Shabaab wanapanga kufanya mashambulizi. Msemaji wa polisi Charles Owino amewataka wananchi kuripoti visa vyovyote ambavyo wanashuku si vya kawaida katika vituo vya polisi. Haya yanakuja wakati Rais Uhuru Kenyatta akisema nchi yake haitaondoa wanajeshi wake nchini Somalia hadi nchi hiyo inayokumbwa na matatizo itakapopata amani, uthabiti na usalama.
Akinukuliwa na vyombo vya habari, Msemaji wa Polisi Charles Owino amesema kuwa katika majuma mawili yaliyopita, wanamgambo wa Al Shabaab wamekuwa wakifanya mikutano katika mpaka wa Kenya na Somalia. Hilo limetokana na hatua ya wanajeshi wa muungano wa kulinda amani wa AMISOM kuvamia ngome zao katika taifa la Somalia. Duru nyingine zinaeleza kuwa Oktoba 13 wanamgambo wa Al Shabaab waliitwa na kamanda wao Abdirahman Fillow katika eneo la El Ade, ambaye anasemekana kuwaleta pamoja wapiganaji 400.
Wanajeshi wa Kenya kuendeleza operesheni Somalia
Wanajeshi wa Kenya walijiunga na kikosi cha kudumisha amani nchini Somalia cha AMISOM mwaka 2011, baada ya taifa hilo kukumbwa na msukosuko wa muda mrefu. Hata hivyo, mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanamgambo wa Al-Shaabab yamesababisha wanajeshi kadhaa kuuawa, hali ambayo mara nyingi huibua mjadala wa kukirejesha kikosi hicho. Rais Uhuru Kenyatta anashikilia kuwa kazi bado ipo:
"Tutaendelea kukita kambi, nchini Somalia chini ya kikosi cha AMISOM hadi malengo yetu ya usalama na yale ya jamii ya kimataifa yatimizwe, yakiwemo ya kurejesha amani na uthabiti nchini Somalia."
Rais aliyasema hayo wakati wa kuadhimisha siku ya wanajeshi nchini Kenya. Katika siku hiyo, taifa huwakumbuka wanajeshi walioaga dunia wakiwa kazini kuitetea, kulinda hadhi, usalama, mipaka na uhuru wa nchi. Rais alisema Wakenya wanajivunia na kuridhishwa na jukumu muhimu linalotekelezwa na wanajeshi katika shughuli za kudumisha usalama katika eneo hili hasa katika kukabiliana na magaidi, changamoto ambayo imeendelea kuzua hofu na wasiwasi miongoni mwa Wakenya:
"Kanda yetu inaendelea kukabiliwa na changamoto, zinazosababishwa na mitandao ya kigaidi, inayokuzwa katika upembe wa Afrika, mitandao hii inaendelea kulenga watu wetu ili kuwahofisha na kuathiri maisha yao ya kila siku."
Wakati wa sherehe hizo, wanawake wa maafisa wajasiri waliopoteza maisha yao wakiwa kazini walikabidhiwa vyeti na vitu vya thamani kwa lengo la kuwatambua waume wao. Waziri wa Ulinzi Rachel Omamo alihudhuria hafla hiyo:
"Nawashukuru wote kwa kuwatoa wapendwa wenu, kuhudumia taifa, tunajiunga nanyi wakati huu mgumu, tunapowakumbuka wale mliowapoteza na wale waliojitolea mhanga."
Kikosi cha wanajeshi wa Kenya kilichoko Somalia kinatarajiwa kuondoka Somalia katika kipindi cha miaka miwili ijayo kwa mujibu wa ratiba ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mhariri: Mohammed Khelef