Kenyatta, Odinga wapinga mishahara minono kwa wabunge
25 Agosti 2017Suala la mishahara ya wabunge limerejea tena midomoni mwao baada ya kutishia kususia vikao na kukwamisha shughuli iwapo hawatalipwa kiwango cha muhula uliopita. Hali hiyo imemlazimu Rais Uhuru Kenyatta kushikilia kuwa hatoupa ridhaa mswada wa kuidhinisha mishahara ya wabunge kuongezwa iwapo utawasilishwa kwake.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga naye pia amejitenga na kauli za wabunge wa vyama vinanavyounda muungano wa NASA wanaoisukuma hoja hiyo.Tume ya mishahara ya wafanyakazi wa umma iliipunguza mishahara ya wabunge miezi 2 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.
Uhuru, Odinga wajitenga na madai ya wabunge
Wabunge wapya nchini Kenya wanasubiri kuapishwa rasmi kabla ya kikao chao cha kwanza kufanyika wiki ijayo. Hata hivyo, baadhi wanatishia kukwamisha shughuli za bunge hususan kuridhia orodha ya baraza la mawaziri itakayopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta. Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta anashikilia kuwa hatoupa ridhaa mswada wa kuuongeza mshahara wa wabunge iwapo utawasilishwa kwake.
"Namuomba kakangu Raila..tafadhali hata pale ulipo…ikiwa mahakama ya juu itaamuru umeshinda nawewe pia usikubali (kuongeza mishahara) ndio wajue hii maneno haiwezekani. Hatuwezi…hatuwezi…pesa ya umma ni mali ya wananchi…lakini sio kuingia mifuko ya wakubwa," alisema rais Kenyatta.
Msimamo huo unaungwa mkono na kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyejitenga na kauli za wabunge wa vyama vinavyounda muunganao wa NASA wanaoisukuma hoja ya kuwaongezea mishahara. Itakumbukwa kuwa miezi 2 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tume ya kusawazisha mishahara ya wafanyakazi wa umma, SRC, inayoongozwa na Sarah Serem iliipunguza mishahara ya wabunge wa Kenya kutokea shilingi laki 710 hadi laki 621,250 pamoja na marupurupu ya kuhudhuria vikao bungeni.
Wabunge wanaaminika kuwa na dhana kwamba wana uwezo wa kuikaba koo serikali kuwaongezea mishahara na marupurupu yaliyofutiliwa mbali na tume ya kusawazisha mishahara ya umma SRC. "Kisheria wabunge hawawezi kufanya kitu….kubadilisha mishahara yao.Lakini ninachojua wanaweza kufanya ni kuwatisha wakuu wa tume ya SRC inayoongozwa na Sara Serem kuwarekebishia miashahara," anasema Ken Mbaabu, mwanasheria wa mjini Nairobi.
Ni wiki hii tu ambapo mwakilishi wa wanawake mteule katika kaunti ya Kiambu Gathoni wa Muchomba alitoa matamshi yaliozusha hisia kali miongoni mwa Wakenya aliposema kuwa anastahili kulipwa vizuri kwani alipigania kiti hicho na ni haki yake. Maneno hayo yaliwakera wakazi wa nje na ndani ya kaunti anayowakilisha ya Kiambu na kulazimika kuomba radhi.
Wananchi wasema basi
"Tutakachofanya ni heri tu waondolewe …wale ambao wanatosheka na hicho kiwango cha biashara wachukue kazi," alisema mfanyabiashara aliejitambulisha kwa jina moja la Antony. " …kuhusu mshahara walikuwa wanajua kiwangowalichopaswa kupata. Mwananchi wa kawaida ndiyo anaumia maana pesa inatoka mfuko wa mwananchi na kwenaenda kwao," alisema mwananchi mwingine Melpha magoma.
Tume ya kusawazisha mishahara ya umma, SRC, imeyafutilia mbali pia marupurupu ya usafiri wa magari ya wabunge na badala yake kuzindua mfumo wa kugharamia usafiri kwa kuzingatia maeneo na mipaka maalum. Mishahara ya maspika wa mabunge imepunguzwa pia kwa shilingi laki 165.
Marupurupu ya kuhudhuria vikao vya kamati za bunge yamepunguzwa hadi shilingi alfu 80 kwa wajumbe na laki 128 kwa wenyekiti bila malipo ya usafiri. Kadhalika wabunge watapewa mkopo wa shilingi milioni 7 kununulia magari badala ya ufadhili wa shilingi milioni 5. Mikopo ya nyumba ya shilingi milioni 20 bado ipo.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya - DW, Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef