Kenyatta ndiye rais mpya wa Kenya
9 Machi 2013Shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura imechukua muda wa siku tano baada ya kura hiyo kupigwa siku ya Jumatatu.
Kuchelewa huko kulitokana na hitilafu iliyosababishwa na kukwama kwa mfumo wa elektroniki wa kujumlisha kura na kuwasilisha matokeo kupitia runinga.
Kama hakutakuwa na mabadiliko, Uhuru Muigai Kenyatta atatangazwa mshindi wa kura hiyo baada ya kupata jumla ya kura milioni 6,173,433 huku mpinzani wake wa karibu Raila Amolo Odinga akimfuatia kwa karibu kwa kukusanya kura 5,340,546. Shughuli ya kujumlisha kura ilikamilika saa nane usiku na wawakilishi wa wagombea urais walianza zoezi la kuthibitisha hesabu hizo.
Kura hiyo ambayo matokeo yake yalisubiriwa kwa kwa hamu imehusisha wagombea wanane ambao ni Waziri Mkuu Raila Odinga Manaibu wake wawili Uhuru Kenyatta na Musalia Mudavadi, James Ole Kitiapi Peter Keneth, Martha Karua, Mohammed Abduba Diba na Wakili Paul Muite.
Kura ya hasira dhidi ya ICC?
Dr. David Matsanga, mtaalamu wa usuuhishi wa migogoro, ameulezea ushindi wa Kenyatta kama kura ya hasira dhidi ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC iliyowafungulia mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu, Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto.
Uchaguzi huo vilevile ulihushisha wagombea wengine wa viti mbali mbali wakiwemo Magavana, Maseneta, Wabunge, waakilishi wa wanawake na waakilishi wa serikali za majimbo.
Hapo jana kundi moja linalojiita 'African Centre for Governance' lilienda mahakamani kutaka zoez zima la kujumlisha kura lisitishwe kwa madai kwamba shughuli ya uchaguzi ilikumbwa na udanganyifu na kutokana na kukwama kwa mfumo wa elektroniki wa kuhesabu kura.
Hata hivyo Jaji David Majanja wa Mahakama kuu alitupilia mbali ombo hilo na kusema hiyo ni kazi ya mahakama ya juu yaani Supreme Court.
Kwa mujibu wa katiba Rais Mpya atakayetangazwa hivi leo ataaapishwa siku kumi na nne zijazo.
Mwandishi: Alfred Kiti, DW-Nairobi
Mhariri: Josephat Charo