Rais Kenyatta na Odinga wafanya mazungumzo
9 Machi 2018Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kinara wa upinzani Raila Odinga wamefanya mazungumzo siku ya Alhamisi katika ofisi ya rais jijini Nairobi kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu ufanyike mwaka uliopita. Rais na kiongozi huyo wa upinzani hao wameafikiana kuweka kando tofauti zao za kisasa na badala yake kujenga taifa. Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika taifa liligawanyika kkabila huku upinzani ukishikilia kuwa hutambui rais Kenyatta.
Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Muungano Mkuu wa upinzani NASA, Raila Odinga umefanyika huku vinara wengine wa upinzani wakikosekana. Muungano wa Nasa umekuwa ukitaka mazungumzo na upande wa serikali bila ya mafanikio suala ambalo limeligawanya taifa kwa makabila. Rais Kenyatta ambaye pia hakuonekana na naibu wake William Ruto amesema, "taifa hili la Kenya ni kubwa kuliko mtu yeyote binfasi." Ameoongeza kusema, "viongozi lazima waje pamoja."
Muungano wa NASA ulisusia uchaguzi
Muungano wa NASA ulisusia uchaguzi ambao Kenyatta alishinda kwa asilimia 98 baada ya kushikilia kuwa palihitajika mageuzi katika tume ya kusimamia uchaguzi. Hata hivyo mageuzi hayo hayakufanyika. Katika hatua ya kuonyesha kutotambua rais Kenyatta, Odinga alijiapisha katika bustani ya Uhuru, huku wafuasi wake wakijitokeza kwa wingi.
Uchumi wa taifa la Kenya ambao ni mkubwa katika kanda ya Afrika Mashariki, umekuwa ukidorora kwa kiwango cha asilimia 4.8 kutoka asilimia 5.8 mwaka 2016 kutokana na mizozo ya kisiasa. Mkutano wa Kenyatta na Odinga ambao ulidumu kwa zaidi ya saa mbili huenda ukachangia kurejesha taifa kwenye mhimili wa ukuaji wa uchumi tena na utangamano. Hata hivyo wanahabari hawakuruhusiwa kuuliza maswali.
Hotuba ya rais Uhuru Kenyatta inajiri huku waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson akizuru nchi hiyo. Majuma mawili yaliyopita aliyekuwa balozi wa marekani nchini Kenya Johny Carson alinukuliwa akisema kuwa Tillerson, alistahili kushinikiza serikali na upinzani kuzungumza ili kuondoa hali ya wasiwasi kwenye ziara yake.
Msemaji wa Odinga Dennis Onyango ameliambia shirika la habari la Reuters, "hapakuwa na shinikizo za mataifa ya Magharibi, hasa Marekani kwa viongozi hao wafanye mazungumzo."
Aidha mkutano wa viongozi hao wawili unajiri huku ripoti ya kituo cha Carter ambacho kilishuhudia uchaguzi mkuu uliopita kikitoa ripoti yake. Kituo hicho kimesema kuwa uchaguzi hukuwa huru na wa haki hasa kwenye kujumilisha kura. Odinga amesema, "tumesema kuwa mgawanyiko ambao umekuwa nasi tangu wakati wa uhuru utaisha nasi sasa."
Marekani, mataifa mengine pamoja na makundi ya kidini yamekuwa yakishinikza kufanyakika kwa mazungumzo kwa Odinga kutambua Uhuru Kenyatta kuwa rais aliyechaguliwa kihalali.
Viongozi wa NASA kufanya kikao
Wakati huo huo kiongozi huyo wa upinzani atakutana na waziri wa masuala ya kigeni wa marekani Rex Tillerson jioni hii. Kwa mujibu wa wizara ya masuala ya kigeni ya Kenya, ratiba ya Tillerson haikuwa imejumuisha kiongozi wa upinzani.
Wabunge wa upinzani wamekuwa wakisusia kuhudhuria vikao vya bunge, suala ambalo sasa huenda likabadilika. Hata hivyo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari viongozi wengine wa Muungano wa NASA Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Musalia Mudavadi wa chama cha ANC na Moses Wetangula wamesema kuwa mkutano kati ya Odinga na Rais Kenyatta umefanyika bila ya wao kuwa na habari. Wameitisha kikao na waandishi habari siku ya Jumatatu ambapo wataelezea msimamo wao.
Itakumbukwa wakati Odinga alipojiapisha viongozi hao hawakuhudhuria na hadi leo hakuna sababu zilizotolewa kwa hatua yao ya kutohudhuria hafla hiyo.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman