Kenyatta ataka Kenya ijitegemee zaidi
27 Machi 2014Hotuba ya rais Kenyatta ilijikita katika mambo makuu matatu yakiwemo wajibu wa Kenya kikanda na kimataifa, hali ya usalama na maadili ya taifa, na kanuni za utawala bora.
Hotuba hiyo ya rais Kenyatta imetolewa wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo matumizi makubwa ya serilai, hali tete ya usalama, na shinikizo kwa nchi hiyo kutimiza wajibu wake wa kimataifa.
Kenyatta alisema serikali yake imetekeleza matakwa ya raia kwa kuanzisha mfumo wa serikali za majimbo, ambapo kaunti 47 zinafanya kazi sambamba na serikali kuu.
Rais Kenyatta alizungumzia azma ya serikali yake kuhakikisha umoja wa kitaifa, usalama wa raia na kulinda uhuru na heshima ya taifa la Kenya, na kuongeza kuwa wakati serikali ina jukumu la kushughulikia mahitaji ya raia, inao pia wajibu wa kushughulikia mahitaji ya mataifa jirani, hasa pale uhuru wa majirani unapokuwa unatishiwa na migogoro ya ndani na ugaidi.
"Ndiyo maana wanajeshi wetu wako nchini Somalia, wakiisaidia kurejesha utawala wake wa sheria na utulivu. Ndiyo maana tumekuwa msitari wa mbele katika juhudi za kuhimiza amani na upatanishi nchini Sudan Kusini.
Na ndiyo maana tumetimiza wajibu wetu wa kimataifa kuyasaidia makundi ya walio hatarini zaidi, tukiopekea wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, ambao wengi wao ni wa asili ya kanda hii."
Azungumzia sera ya kujitegemea
Rais Kenyatta alisema baadhi ya matatizo hasa ya kiuchumi inayoendelea kukabiliana nayo Kenya ni matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji usiyokidhi mahitaji katika miongo mitatu iliyopita.
Lakini akasema ni jukumu la serikali yake kuyatafutia ufumbuzi kwa kuzingatia maadili ya kikatiba ya uwazi na ushirikishaji wa umma. Kenyatta amesema utawala wake unaamini kwamba Kenya inahitaji kujenga uwezo wake wa kitaifa ili kufadhili yenyewe miradi yake ya maendeleo.
"Ni kwa sababu hii tumetanua maeneo ya kukusanya kodi ya ongezeko la thamani VAT. Najua kuwa hili linaweza kuwa limepokelewa kama kuongezwa kwa gharama za maisha na kwamba linawaumiza raia.
Napenda kusisitiza kwamba ingawa jambo hili linaweza kusababisha makali ya maisha katika kipindi kifupi, lakini litasaidia ustawi wa taifa letu katika kipindi cha muda mrefu," alisema Rais Kenyatta.
Kenyatta pia alizungumzia azma ya serikali yake kuwezesha mapinduzi katika sekta ya teknolojia ya mawasiliano na habari, kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa chakula, ambapo ameelezea dhamira ya serikali kutenga ekari milioni moja kwa ajili ya kilimo cha umuagiliaji ili kuchana na kilimo cha kutegemea mvua pekee.
Kuhusu sera ya Kigeni, rais Kenyatta alisema wanaungana na mataifa wanachama wa jumuiya ya Afrika mashariki, ambapo kupitia ushirikiano huo, mshikamano wao unakwenda mbali katika mataifa mengine ya bara la Afrika.
Alisema ziara zake katika mataifa ya Nigeria, Ethiopia, Angola na Afrika Kusini zimemuonyesha kuwa viongozi na watu wa bara hili sasa wamezinduka kikamilifu kuhusu uwezo wa Afrika.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.