Kenyatta aonya wanaotaka kuleta vurugu
20 Oktoba 2017Wakenya walijitokeza kwa wingi kuikumbuka Siku ya Mashujaa, kuwaenzi vigogo waliyoikomboa nchi kutokana na ukoloni. Katika hafla ya ya mwaka huu rais Kenyatta alizungumzia masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuahidi kuanzisha baraza litakaloshughulikia matakwa ya mashujaa. "Naomba kutangaza kwamba tunapanga kuanzisha baraza la mashujaa, litakalokuwa na jukumu la kutambua na kupata majibu ya masualaya ustawi na uungaji mkono wa mashujaa wetu," alisema Kenyatta.
Akitoa hotuba yake kwa taifa katika uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi, Kenyatta ameongeza kwamba serikali yake imeweka kima cha shilingi bilioni 25 kwa mfumo wa masomo ya bure ya sekondari inayotarajiwa kuanza mwezi Januari mwaka ujao.
Akizungumzia suala la uchaguzi mpya unaotarajiwa kufanyika Oktoba 26, rais Kenyatta amewaonya wale wanaopanga kuuvuruga kwamba watakutana na mkono wa sheria. Amesema serikali yake imeshaweka vikosi vya usalama nchi nzima kupambana na wale wote watakaojaribu kuvuruga amani.
Pia Kenyatta ametoa onyo kwa wale wanaotoa vitisho kwa maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, akisema vitendo kama hivyo havitavumiliwa au kukubaliwa. "Wakenya wana haki ya kuandamana kama ilivyoandikwa katika katiba yetu, lakini maandamano hayo yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria,” aliongeza rais Kenyatta.
Matamshi yake yalielekea kuulenga muungano wa upinzani NASA uliyoitisha maandamano ya amani wiki ijayo kuipinga tume ya uchaguzi Kenya IEBC, kuendelea na shughuli ya uchaguzi wakidai ni lazima madadiliko ndani ya tume hiyo yafanyike kabla ya kuruhusiwa kuuandaa uchaguzi wenyewe. Maandamano hayo yanatarahjiwa kufanyika siku ambayo wakenya watakapokuwa wanashiriki uchaguzi mpya, baada ya ule uliyofanyika Agosti 8 kufutwa kufuatia madai ya udanganyifu na zoezi zima kutofanywa kuzingatia sheria ya uchaguzi. "Kwa wale wanao watishia maafisa wa tume ya IEBC hii ni lazima ikome tunapaswa kuamini, kuimarisha na kulinda taasisi zetu ili kuziwezesha kukuwa na kufanya kazi vizuri," alisema rais Kenyatta.
Wakati huohuo Kiongozi wa upinzani NASA Raila Odinga akiandamana na wanachama wengine wa muungano huo, wameienzi siku ya mashujaa mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya kwa kuwakumbuka waandamanaji waliyouwawa wakati wa maabndamano ya kuipinga tume ya uchaguzi IEBC. Odinga anatarajiwa kutoa maelezo zaidi siku ya Jumatano kuhusiana na uchaguzi mpya wa Oktoba 26.
Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman