1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta anaongoza katika matokeo ya uchaguzi Kenya

9 Agosti 2017

Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi mkuu wa Kenya yanaendelea yanayonesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta anaongoza na pengo kubwa dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga.

https://p.dw.com/p/2huL4
Kenia Wahlen Präsident Uhuru Kenyatta bei Stimmabgabe
Picha: picture-alliance/abaca/A. Wasike

Mgombea wa uchaguzi wa rais kwa tikiti ya muungano wa upinzani – NASA Raila Odinga ameyakataa matokeo yaliyotolewa mpaka sasa akisema tume ya uchaguzi inahitajika kisheria kuonyesha fomu zilizotiwa saini na waangalizi wa vyama kutoka kila kituo cha kupigia kura zikiidhinisha matokeo kitu ambacho hakijafanyika. "Fomu namba 34 hazipoaswi kuja baada ya matokeo. Zinapaswa kuandamana na matokeo. Hivyo tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa mpaka sasa, na tunataka IEBC itoe fomu namba 34  kutoka vituo vyote kabla matokeo mengine yote hayajatangazwa" amesema Raila

Badala yake, tume hiyo ya uchaguzi inamwonyesha kwenye tovuti yake, Rais Uhuru Kenyatta akiwa kifua mbele na asilimia 55 ya kura dhidi ya Odinga ambaye ana asilimia 44 baada ya karibu robo tatu ya vituo vya kupigia kura kuwasilisha matokeo yao.

Kenia Raila Odinga PK in Nairobi
Odinga anasema matokeo yanayotolewa sio ya kweliPicha: Reuters/B. Ratner

Hata hivyo, tume hiyo haijatoa habari kuhusu ni majimbo gani yaliyohesabiwa, hivyo haikuwa wazi kujua kama ngome za wafuasi wa Kenyatta au za upinzani, au kutoka pande zote mbili zimehesabiwa au la. Odinga anapinga tarakimu hizo akisema uongozi wa Kenyatta umezusha shaka kwa kuwa umebaki pale pale tangu zoezi la kujumlisha kura lilianza na haziendani na kile ambacho anaambiwa na mawakala wa chama chake ambazo zinaonyesha kuwa wako kifua mbele. Lakini upande wa chama cha Jubilee umepinga kauli ya NASA ukisema muungano huo unakwenda kinyume na uamuzi uliotolewa na mahakama baada ya wao wenyewe kuwasilisha kesi mahakamani wakitaka matokeo yanayotangazwa katika kituo cha kupigia kura yawe ndiyo ya mwisho. Raphael Tuju ni Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee "Tunaona wao sio wakweli. Kwa wao sasa kubadilisha msimamo wao. Sidhani kama unaweza kubadilisha sharia wakati mchakato ukiendelea. Sheria ni sheria na lazima sote tuziheshimu"

Kamishna wa IEBC Rosyln Akombe amesema kuna chama ambacho hakukitaja, kilichopinga kutolewa kwa matokeo hayo, lakini kama tume wameamua kuendelea kuyatangaza "Tumeamua kama tume kuwa tutaendelea kutoa matokeo, ili vyombo vya habari, na wakenya wawe na fursa ya kuendelea kupata matokeo, na pia tunaamini hio ni kuheshimu sheria tulizo nazo na pia uamuzi uliofanywa na mahakama" Amesema Akombe

Kenia Ezra Chiloba Leiter der Wahlkommission
Tume ya uchaguzi inaendelea kutoa matokeo ya awaliPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Chini ya katiba ya kenya, matokeo ya kila kituo cha kupigia kura yanapaswa kujazwa kwenye fomu ambayo inatiwa saini na waangalizi kutoka kila chama katika kituo hicho, kisha kuchapishwa na tume ya uchaguzi kwenye tovuti ya umma. Hatua hiyo inapaswa kusaidia kuhakikisha kuwa uchaguzi haufanyiwi mizengwe na vyama vinaweza kuthibitisha matokeo.

Odinga aligombea katika chaguzi mbili zilizopita na akashindwa zote, ambapo alitoa madai ya wizi w akura kufuatia dosari zilizojitokeza katika chaguzi hizo. Katika mwaka wa 2007, wito wake wa kufanyika maandamano ulizusha machafuko ya kikabila ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200. Katika mwaka wa 2013, alituliza ghasia kwa kuwasilisha malalamiko yake mahakamani.

Mshindi wa kinyang'anyiro cha urais lazima apate Zaidi ya asilimia 50 ya kura pamoja na robo moja au kura Zaidi katika karibu kaunti 24 kati ya 47 za Kenya, kwa mujibu wa maafisa. Kama mgombea anayeongoza hatoweza kutimiza kiasi hicho, wagombea wawili wakuu wataingia katika duru ya pili ya uchaguzi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Zainab Aziz