1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta akataa ongezeko la VAT la asilimia 16

Daniel Gakuba
14 Septemba 2018

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amependekeza kupunguzwa kwa ushuru unaotozwa bidhaa za mafuta kwa asilimia 8 kutoka asilimia 16. Kwenye hotuba kwa taifa, amelitaka bunge kuufanyia marekebisho muswada wa Fedha wa mwaka 2018.

https://p.dw.com/p/34tEA
Deutschland Uhuru Kenyatta in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Macho yote ya wakenya sasa yataelekezwa kwenye Bunge, baada ya mapendekezo mapya ya rais kuhusu mswada wa Fedha wa mwaka 2018. Rais Kenyatta alikataa kutia sahihi mswada huo uliofanyiwa marekebisho na bunge hilo Alhamis na badala yake anataka urejeshwe bungeni ufanyiwe marekebisho zaidi. Bunge lilikuwa limependekeza kuahirishwa kutekelezwa kwa ushuru wa asilimia 16 kwenye bidhaa za mafuta hadi mwaka 2021. Rais akiwalaumu wabunge kwa kushindwa kuangalia maslahi mapana ya wakenya walipopitisha mswada huo ulipowasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2013.

"Nimependekeza kupunguzwa kwa ushuru wa ongezeko la thamani -VAT kwa asilimia 50, kumaaninisha kutoka asilimia 16 hadi nane, iwapo bunge litaafiki mapendekezo haya, bei mpya ya petroli itakuwa shilingi 118 kutoka shilling 127 na bei ya dizeli itapungua kutoka shilingi 118 hadi shilingi 107.” Amesema Kenyatta katika hotuba yake.

Shimo linalomeza fedha za umma

Akitambua fika kuwa ufisadi ni zimwi ambalo humeza kiasi kikubwa cha fedha za serikali, rais Kenyatta amependekeza kuongezewa fedha kwa idara ya mahakama ili kuharakisha kuamuliwa kwa kesi zinazowakabili mafisadi. Idara ya mahakama ilikuwa imeomba kutengewa shilingi bilioni 31.2 na badala yake ikatengewa shilingi bilioni 17.3 kwenye bajeti ya mwaka huu.

Kenja Proteste gegen Korruption an Unabhängigkeitstag
Waandamanaji wanaopinga ufisadi nchini KenyaPicha: picture alliance/dpa/D. Kurokawa

Habari hizo ni za kutia moyo baada ya Jaji Mkuu David Maraga kuwakejeli wabunge kwa kukosa kutambua umuhimu wa idara ya mahakama hivyo kuitengea fedha kidogo. Margaret Kamar  mbunge wa chama tawala cha Jubilee, amesema wanasubiri muswada urudi bungeni.

''Bunge litatoa kauli yake kuhusu suala la ushuru wa ongezeko la thamani. Tunajua wengi wetu wanateta kuwa kodi hiyo ya asilimia 16 imechukua muda mrefu. Huu ni wakati mgumu kwa wakenya kwa hivyo tunatarajia kuwa hilo litatimizwa.'' Amesema mbunge huyo.

Nyongeza ya asilimia 16 katika ushuru wa VAT yawatesa Wakenya

Wafanyibiashara wametakiwa kupunguza bei za bidhaa zao kufuatia kutekelezwa kwa ushuru huo wa asilimia 16 ambao umesababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha. Lakini hilo litafanyika tu wakati bunge litafanyia marekebisho mswada huo na rais kuuidhinisha kwani kulingana na sheria, nyongeza ya ushuru ya asilimia 16 inatekelezwa kwa sasa.

Kenia - Stoffbeutel in Markt
Kuongezeka kwa ushuru wa VAT kumepandisha gharama ya maisha nchini KenyaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim

Pamoja na habari hiyo njema, bajeti ya taifa inakabiliwa na nakisi, kwani ushuru wa asilimia 16 ulilenga kukusanya shilingi bilioni 30. Hivyo rais amependekeza kupunguzwa kwa matumizi kwenye sekta mbali mbai:

Amesema, "Kupunguza matumizi kwenye sekta hiyo kunalenga matumizi ya fedha yasiyo ya lazima kama vile sekta ya huduma, safari za nje na ndani ya nchi, mafunzo na semina, hali hii inamanisha kuwa sisi sote kwenye serikali tukaze mikanda yetu.”

Wakati huo huo Shirika la Fedha Ulimwenguni –IMF, limetoa hakikisho kwa taifa la Kenya kuwa litaendelea kuliunga mkono kwenye miradi ya maendeleo yake. Hayo yamesemwa na mwakilishi wa shirika hilo nchini Jan Mikkelsen. Mikkelsen amesema kuwa nafasi ya Kenya katika kanda hii ni muhimu na kwamba akiba ya viwango vyake vya fedha za kigeni ni nzuri.
 

Mwandishi: Shisia Wasilwa/Dw, Nairobi

Mhariri: Daniel Gakuba