Kenyatta akataa kusaini kitita cha pensheni ya wabunge
11 Septemba 2020''Sasa mwananchi ni maskini. Hana hata pesa ya kununua chakula, lakini akifungua gazeti anaona wabunge wamejiongezea mishahara, kwa sababu kama ingekuwa hivyo, huyo mwanachi hangekuwa na shida hata kama unajilipa shilingi milioni moja.'' Alisema Rais Kenyatta hapo jana (Septemba 10) mara baada ya kikao cha baraza lake la mawaziri jijini Nairobi.
Endapo sheria hiyo ambayo rasimu yake iliwasilishwa bungeni na Kiongozi wa Wachache, John Mbadi, ingeliidhinsihwa na Rais Kenyatta, basi ingemgharimu mlipa kodi takribani shilingi 444,000,000 kila mwaka.
Lakkini wakati akiitetea rasimu ya ya mswada huo alipouwasilisha bungeni, Mbadi alisema wabunge waliostaafu wanapitia changamoto nyingi kutokana na ugumu wa maisha.
Mbunge huyo wa Suba Kusini aliitaka serikali kuanza kuwalipa wabunge hao waliostaafu kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.
Hata hivyo, wakati wabunge wakiwateteta wenzao, madaktari na matabibu wanaohudumu kwa sasa wamegoma wakitaka nyongeza ya mshahara na mazingira bora na hakuna mbunge ambaye ameonekana kuwatetea.
Pingamizi la serikali
Mswada huo ulipata pingamizi kutoka kwa wizara ya Fedha na Tume ya Kusimamia Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma nchini Kenya. Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Mishahara ya Wafanyikazi wa Umma, Lynne Mengich, alisema Kenya inatumia shilingi bilioni 895 kwa mishahara ya wafanyakazi wa umma kila mwaka, hali "inayomaanisha kuwa hatuna fedha zaidi za kufanyia shughuli za kimaendeleo na huduma nyingine."
Aliyekuwa kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa, Aden Duale, akishikilia kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi katika sekta za umma pia wakafuata mkondo huo wa kutaka malipo yao ya kustaafu yaongezwe.
Tume hiyo ilihoji kuwa, mtu anapofanya kazi anastahili kulipwa kulingana na jinsi alivyokuwa akiweka kwenye mfuko wa kustaafu. Kwa sasa wabunge hao waliohudumu kati ya mwaka 1984 hadi mwaka 2000, wanapokea shilingi elfu sita.
Tayari Baraza la Magavana pia linataka mafao makubwa ya pensheni pindi magavana watakapokamilisha hatamu zao majimboni. Bunge la Seneti pia limependekeza wabunge wa majimbo kulipwa shilingi milioni 1.5 za Kenya na pensheni ya shilingi elfu thelathini kila mwezi, pindi watakapokamilisha mihula yao ya kuhudumu.
Wabunge wa Kenya ni miongoni mwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ulimwenguni, huku kila mbunge akipokea euro 10,000 kwa mwezi, mbali na marupurupu yanayofikia shilingi milioni moja za Kenya.
Imetayarishwa na Shisia Wasilwa, DW Nairobi